Huwa tuna mipango mbalimbali tunayofanyia kazi kwenye maisha yetu, katika kufika kwenye mafanikio tunayotaka kufikia.
Lakini mara nyingi tumekuwa tunajikwamisha wenyewe pale tunapolazimisha matokeo fulani yatokee kwa wakati ambao tunataka sisi.
Yaani tunajipangia wenyewe hatua tutakazochukua na matokeo ambayo tunataka kuyapata kwa muda ambao tunapanga kupata matokeo hayo.
Tunajituma kweli kweli kuchukua kila hatua ambayo tunapaswa kuchukua lakini hatupati matokeo ambayo tulitegemea kuyapata kwa muda tuliopanga.
Hapa ndipo wengi wanapokata tamaa na kuona hawawezi kufanikiwa kwenye maisha yao, labda hawana bahati au dunia haiwajali.
Na hilo ni kosa kubwa sana, kwa sababu ukifikia kukata tamaa kwa sababu unaweka juhudi kubwa na huoni matokeo uliotegemea kuona kwa wakati uliopanga kuona, unajizuia mwenyewe kufanikiwa.
Jukumu lako kuu ni kuifanya kazi yako, kuchukua zile hatua ulizopanga kuchukua, na kuendelea kufanya hivyo mara zote.
Kwa kufanya kazi yako, utapata matokeo ambayo ni bora sana, lakini huwezi kudhibiti matokeo hayo yanakuja muda gani. Yanaweza kuja mapema kuliko ulivyotegemea au mara nyingi yakaja yamechelewa kuliko ulivyotarajia.
Unachopaswa kuelewa ni kwamba kwa kuweka kazi utapata matokeo ya tofauti, japo huwezi kudhibiti ni kwa wakati gani matokeo hayo yatapatikana.
Hivyo rafiki yangu, kitu muhimu cha kuondoka nacho hapa leo ni hiki, ifanye kazi yako kwa usahihi, umakini na kujituma sana. Kisha iache dunia nayo ifanye kazi yake katika kukuletea matokeo bora. Usilazimishe kupata matokeo bora kwa muda unaotaka wewe, dunia haijali sana kuhusu wewe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,