Rafiki yangu mpendwa,
Juma namba 28 la mwaka huu 2019 linatuacha, hatutakuwa na muda kama huu tena kwenye maisha yetu. Lakini yale tuliyojifunza na kufanya kwenye juma hili yatabaki na sisi milele kwenye maisha yetu. Kumbuka kila unachofanya au kutokufanya kwenye maisha yako kinaacha alama fulani kwako. Hivyo tumia vizuri sana muda wako kwa kuweka vizuri vipaumbele vyako vizuri.
Juma hili tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa Stand Out: How to Find Your Breakthrough Idea and Build a Following Around It ambacho kimeandikwa na Dorie Clark.
Wote tunajua ni kwa namna gani ushindani umekuwa mkali kwenye zama tunazoishi. Kutokana na ukuaji wa teknolojia na mtandao wa intaneti, chochote unachofanya siyo tu unashindana na wanaokuzunguka, bali unashindana na dunia nzima. Hivyo kama huna mbinu za kukutofautisha na wengine, hutaweza kufanikiwa.
Kwenye kitabu cha STAND OUT mwandishi anatushirikisha jinsi ambavyo tunaweza kujitofautisha na wengine kwa kile tunachofanya. Mwandishi anatufundisha njia ya kubobea sana kwenye kile tunachofanya kwa namna ambayo tutakuwa viongozi ambao wengine wanatuangalia na kujifunza kutoka kwetu (thought leader).
Mwandishi ametumia mifano ya watu mbalimbali ambao wameweza kujitofautisha sana kwa kujijengea ubobezi wa kipekee kwenye kile wanachofanya na kuweza kufanikiwa sana.
Karibu kwenye tano hizi za juma, ujifunze njia sahihi za kubobea kile unachofanya na kuweza kujitofautisha kabisa na wengine.
#1 NENO LA JUMA; DUNIA INATAKA KUKUSIKIA.
Rafiki yangu mpendwa, leo hii nataka kukuambia kitu kimoja muhimu sana ambacho huenda hujawahi kuambiwa au kufikiria.
Kitu hicho ni kwamba dunia inataka kukusikia. Dunia ina hamu kubwa ya kusikia kutoka kwako, kusikia kile kilichoujaza moyo wako. Kwa sababu kupitia kile utakachosema wewe, dunia itakuwa bora zaidi ya ilivyo sasa.
Najua kwa kusikia maneno haya unaweza kusema siyo kweli, kwamba wewe huna cha kuiambia dunia.
Lakini nikuambie kitu kimoja, kila mmoja wetu ana kitu cha kusema, kitu ambacho akikisema basi dunia itanufaika sana.
Inawezekana unachotaka kusema ni kuhusu malezi, kwamba kwa namna malezi yanafanyika sasa unaona siyo sawa, hivyo unafikiri ipo njia bora zaidi ya kufanya malezi. Dunia ingependa sana kusikia kutoka kwako.
Inawezekana unataka kusema kuhusu uongozi, kwamba kwa namna watu wengi wanaendesha nafasi za uongozi wanazopewa siyo sahihi na hivyo unaona kuna njia bora zaidi ya kuongoza. Dunia ipo tayari kukusikiliza kwa hilo.
Inawezekana pia unataka kusema kuhusu fedha, kwa kuwaangalia wengi wanavyohangaika kwenye eneo la fedha, unaona ipo njia bora ya watu kupata, kutunza na hata kuzalisha fedha zao na wakaondokana na changamoto za kifedha. Dunia ipo tayari kukusikiliza kwa hilo.
Kwa chochote kile ambacho unakijua, unapenda kukifuatilia, umekisomea au una uzoefu nacho, dunia inahitaji sana mchango wako katika kufanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi.
Hivyo ni wakati wako sasa kusema, kuifanya dunia ijue kile ambacho ni sahihi kufanyika.
Watu wengi wamekuwa wanakwama kwenye usemaji, wengi wakijiona hawana namna ya kusema wakasikika. Wengi hufikiria kama wangepewa nafasi kubwa ya uongozi basi wangetoa mawazo yao mazuri. Wengine wanafikiri kama wangepata nafasi kwenye vyombo vikubwa vya habari, basi wangetoa mawazo yao ya uboreshaji zaidi.
Lakini ambacho wengi wanasahau ni kwamba kwa zama tunazoishi sasa, kila mtu ni chombo cha habari na kila mtu ni kiongozi.
Hapo ulipo, una fursa nzuri ya kuweza kuipa dunia mawazo yako mazuri kwa njia ambazo ni rahisi kabisa na ambazo zinaweza kuwafikia wengi.
Unaweza kutumia mitandao ya kijamii kutoa mawazo yako bora kwa wengine, unaweza kuwa na blog ambayo unaitumia kuandika mawazo yako, lakini pia unaweza kuandika kitabu na kukitoa kwa mfumo wa nakala tete (softcopy) na kikawafikia wengi sana bila ya kuingia gharama za uchapaji.
Hivyo rafiki, ni wakati wako sasa kuipa dunia kile ambacho inakosa. Hebu anza kwa kuyaandika vizuri mawazo yako, kwa kile ambacho umekuwa unafuatilia sana, au ulichosomea au ambacho una uzoefu nacho. Shirikisha mawazo yako kupitia mitandao ya kijamii na pia anzisha blog yako ambayo utakuwa unaandika mawazo yako hayo.
Kadiri muda unavyokwenda na unavyozidi kutengeneza wafuasi kwenye mitandao ya kijamii na blogu pia, hapo sasa unaweza kuandika kitabu ambacho unaweza kukitoa bure au kukiuza kwa wasomaji wako.
Kitu muhimu kabisa kujua ni kwamba, kwa kushirikisha dunia kile unachojua, una fursa kubwa ya kutengeneza kipato baadaye. Kwenye kitabu cha juma hili utajifunza yote hayo. Lakini napenda sana uondoke na neno hili muhimu, dunia inataka kukusikia, ni wakati wako sasa kusema kile unachojua ni sahihi. Usikubali kuzuiwa na chochote.
#2 KITABU CHA JUMA; JINSI YA KUTENGENEZA UBOBEZI UTAKAOKUNUFAISHA.
Kama nilivyokushirikisha kwenye utangulizi, juma hili tunakwenda kujifunza kutoka kitabu kinachoitwa Stand Out: How to Find Your Breakthrough Idea and Build a Following Around It ambacho kimeandikwa na Dorie Clark.
Kwenye kitabu hiki Dorie anatupa maarifa sahihi ya kuweza kujitofautisha sana kwenye kile tunachofanya kwa kutengeneza ubobezi. Kwa njia hii, tunakuwa wa tofauti na hivyo kuweza kupiga hatua zaidi.
Kitabu hiki cha STAND OUT kimegawanywa kwenye sehemu tatu muhimu.
Sehemu ya kwanza ni kutafuta wazo ambalo litakutofautisha na wengine. Hapa unakuja na kitu ambacho unakwenda kukibobea na hivyo kuwa tofauti na wengine wanaofanya kitu cha aina hiyo.
Sehemu ya pili ni kujenga wafuasi kwenye wazo lako la tofauti. Hapa unajenga watu ambao wanakubaliana na wazo hilo na hivyo kuweza kwenda na wewe pamoja.
Sehemu ya tatu ni kuweza kufikia mafanikio makubwa kupitia wazo lako hilo na pia kuweza kutengeneza kipato kupitia wazo lako la tofauti.
Karibu kwenye uchambuzi wa kina wa kitabu hiki, ujifunze jinsi ya kuja na wazo la tofauti, kujenga wafuasi kwenye wazo hilo na hatimaye kutengeneza kipato na kufikia mafanikio makubwa.
SEHEMU YA KWANZA; KUPATA WAZO.
Kutokana na urahisi wa sauti ya kila mtu kusikika, kila kitu kimekuwa kama kelele. Kila mtu anaweza kuwa na maoni kwenye jambo lolote lile. Mitandao ya kijamii imejaa taarifa nyingi ambazo hazipati nafasi ya kusambaa na kuwafikia wengi.
Lakini pamoja na wingi huu wa maarifa na taarifa, bado ipo njia ya wewe kuja na wazo ambalo litakuwa la kipekee na kukuwezesha kujitofautisha na wengine na hata kufanikiwa.
Katika kupata wazo bora, zingatia mambo yafuatayo;
Moja; anza na chochote unachojali sana.
Watu wengi wamekuwa wanafikiria kwamba ili uweze kuleta mabadiliko makubwa kwako na kwa wengine basi inabidi uwe na wazo kubwa na la kipekee sana. Wazo ambalo wengine hawajawahi kuwa nalo. Huo siyo ukweli, unaweza kuanza na wazo lolote na ukaweza kulijenga kwa utofauti na ukajitofautisha sana.
Anza na chochote unachojali, unachopenda, unachoamini, unachojua, ulichozoea au ambacho umesomea. Chochote kile ambacho unaona kinaweza kuwa bora zaidi ya kilivyo sasa, unaweza kukichukua kama wazo lako la kufanyia kazi.
Mbili; uliza maswali ambayo hayaulizwi.
Watu wamekuwa wanafanya mambo kwa mazoea kwa sababu wanafanya kile ambacho kila mtu anafanya, na hawathubutu kujaribu vitu vya tofauti. Sasa kwa wazo unalotaka kufanyia kazi kulioresha zaidi, anza kwa kuuliza maswali ambayo watu wengine hawaulizi.
Maswali hayo yanaweza kuwa, vipi kama…. vipi kinyume cha… Hapa unajaribu kupata picha ya tofauti na wengi walivyozoea, kwa kuona upande wa pili wa vitu au kwa namna ya tofauti.
Tatu; angalia uzoefu wako binafsi.
Baada ya kujiuliza maswali ya tofauti kwenye wazo unalotaka kufanyia kazi, angalia uzoefu wako binafsi kwenye wazo hilo. Usijidharau kwa sababu labda huna elimu kubwa au uzoefu mkubwa kwenye jambo hilo. Labda siku za nyuma umewahi kujaribu kufanya tofauti na ukapata matokeo ya tofauti, hiyo inatosha kukuonesha kwamba kuna uwezekano wa kupata matokeo tofauti na ambayo watu wanapata sasa.
Nne; chagua eneo la ubobezi kwenye wazo lako.
Wazo unalokuwa nalo linaweza kuwa pana, sasa unahitaji kuchagua eneo ambalo utabobea kwenye wazo hilo ili kujitofautisha kabisa na wengine. Badala ya kutaka kufanya kila kitu, unachagua eneo moja ambalo utaweka muda na nguvu zako na kuweza kutengeneza ubobezi mkubwa. Ni kupitia ubobezi huu ndiyo unaweza kupiga hatua kubwa kwenye wazo hilo.
Tano; fanya utafiti.
Watu wengi wamekuwa wanapata mawazo mapya ya kuboresha zaidi, lakini hawanufaiki nayo kwa sababu huwa hawaweki kazi inayopaswa kuwekwa ili mtu kubobea kwenye kitu hicho. Moja ya kazi kubwa unayopaswa kuweka ni kufanya utafiti. Siyo kusoma tafiti, badala yake kufanya utafiti mpya, kwa kuangalia yale maeneo ambayo unataka yawe bora kisha kuja na njia bora za kuyaboresha kutoka kwenye tafiti mbalimbali zinazogusa wazo hilo.
Sita; unganisha mawazo.
Kuna maeneo mengine ambayo yameweza kupiga hatua kubwa, ambayo ni tofauti na wazo unalofanyia kazi wewe. hii haikuzuii wewe kujifunza kutoka maeneo hayo. Jifunze kupitia maeneo mbalimbali kwa hatua ambazo watu wameweza kupiga, kisha unganisha mawazo hayo na wazo unalofanyia kazi kuweza kuona jinsi gani ya kuboresha wazo unalofanyia kazi. Kumbuka misingi ya mafanikio kwenye kila eneo inafanana, hivyo kwa kuangalia jinsi ambavyo mawazo mengine yamefanikiwa, utaweza kufanikisha wazo lako pia.
Saba; tengeneza nguzo ya kubeba wazo lako jipya.
Baada ya kuchagua wazo unalotaka kuboresha, ukauliza maswali ya tofauti, ukatumia uzoefu wako, ukafanya utafiti na hata kujifunza kutoka maeneo mengine, unakuwa umejifunza mambo mengi sana kuhusiana na wazo lako jipya. Hapa unakuwa na maarifa na taarifa nyingi ambazo mtu mwingine siyo rahisi kuyaelewa. Hivyo ili wazo lako la kuboresha liweze kueleweka na kutumiwa na wengine, unahitaji kutengeneza nguzo ya kubeba wazo lako. Hapa unatengeneza mfumo unaobeba wazo lako jipya, kwa namna ambayo watu wengine wanaelewa jinsi linavyofanya kazi na matokeo ya tofauti yanavyopatikana.
Kwa hatua hizo saba, unakuwa umekamilisha wazo lako la tofauti, ambalo linaleta matokeo bora kuliko yale ambayo yamezoeleka. Baada ya hapo sasa unakwenda kwenye hatua ya pili ambayo ni kujenga wafuasi kwenye wazo lako.
SEHEMU YA PILI; JENGA WAFUASI KWENYE WAZO LAKO.
Tayari umeshatengeneza wazo lako bora na la tofauti ambalo linaweza kuleta matokeo ambayo ni bora kuliko yale ambayo yamezoeleka. Kumbuka wazo hili haijalishi ni kwenye nini, iwe ni kwenye elimu, uongozi, siasa, afya, biashara, fedha, jamii, chochote kile ambacho unaamini kinaweza kubadilika na kuwa bora, unaweza kuja na wazo lako jipya kwa hatua saba tulizojifunza kwenye sehemu ya kwanza.
Katika kujenga wafuasi kwenye wazo lako, kuna hatua tatu unazopaswa kupitia.
Hatua ya kwanza ni mmoja kwa mmoja.
Hatua ya kwanza katika kutengeneza wafuasi kwenye wazo lako ni wewe mtu mmoja kumfikia mtu mmoja mmoja. Hapa unatengeneza mtandao wako wa watu wanaokujua na kujua kile ambacho unasimamia. Katika hatua hii unahitaji kuchagua wale watu ambao wana ushawishi sana kwenye sekta ambayo wazo lako jipya linahusika. Watu hawa ndiyo wanaokukutanisha na watu wengi zaidi.
Zipo njia mbalimbali za kutumia kwenye hatua hii, zifuatazo ni hizi;
- Kutengeneza kikundi cha watu wanaofanya kile unachofanya, kama ni taaluma, kazi au aina ya biashara unayofanya. Kikundi hiki mnakuwa mnakutana mara kwa mara na kujadili mambo muhimu yanayohusu kile mnachofanyia kazi. Kupitia kikundi cha aina hii unaweza kuimarisha wazo lako na hata kuanza kulisambaza.
- Unaweza kutumia njia ya mahojiano na wale ambao wamepiga hatua zaidi ili kujifunza kwao na hata kukuza mtandao wako kupitia mtandao wao. Watu ambao wamefanikiwa huwa hawana muda wa kumpa kila mtu. Sasa wewe unaweza kuwa mbunifu, ukaanzisha kipindi cha mahojiano (podcast) na kukitumia kuomba kuwahoji wale ambao wamepiga hatua. Wengi wanakubali mahojiano na hapo sasa unajifunza kutoka kwao na kuweza kuwafikia wengi pia kupitia wazo lako.
- Tumia mahusiano yako ya nyuma kuweza kukuza mtandao wako. Mfano wa mahusiano haya ni watu uliosoma nao pamoja, watu mliotoka eneo moja, watu mliowahi kufanya kazi kwenye kampuni moja na kadhalika. Unapotumia mahusiano ya nyuma inakuwa rahisi kuwashawishi watu kukubaliana na wewe.
- Shughuli za kijamii kama kujitolea au kushiriki matukio ya kijamii ni njia nyingine bora unayoweza kutumia kukuza mtandao wako na kuwafikia watu ambao unawalenga kuwafikia kwa wazo lako.
Njia zote hizi nne zinakusogeza karibu zaidi na watu wenye ushawishi kuhusu wazo ulilonalo na hata wale ambao wanaweza kulitumia au kulisambaza zaidi kwa wengine.
Hatua ya pili ni mmoja kwa wengi.
Baada ya kutengeneza mtandao wako wa wale watu unaowajua na wanaokujua, ambao wanakuwa upande wako na kukusaidia kwenye kusambaza wazo lako, sasa unahitaji kusambaza wazo lako kwa watu wengi zaidi. Hapa unatengeneza mtandao wa watu ambao wanakufuatilia na kujifunza kutoka kwako, na hivyo kuweza kutumia wazo lako jipya katika kuboresha zaidi maisha yao na kile wanachofanya.
Katika kuwafikia watu wengi zaidi tumia njia zifuatazo;
- Kuwa na blogu ambayo unaandika kuhusiana na wazo lako. Blogu ni njia rahisi kabisa ya kuweka mawazo yako kwenye mtandao ambapo mtu yeyote duniani anaweza kuyafikia. Hivyo unapaswa kuwa na blogu ambayo unatumia kuandika kuhusu wazo lako na kuwafikia wengi zaidi.
- Tumia mitandao ya kijamii. Kwa sasa watu wengi sana wapo kwenye mitandao ya kijamii. Na hata wale wasiotembelea blog, bado wanatembelea mitandao ya kijamii. Hivyo unapotaka kusambaza wazo lako, unapaswa kutumia pia mitandao ya kijamii. Kuwa na mitandao ya kijamii hakuwi mbadala wa blog. Badala yake unakuwa na blog, kisha unashirikisha maarifa yaliyopo kwenye blog kwa kutumia mitandao ya kijamii. Hivyo unaweza kuandaa jumbe fupi fupi, picha na mafunzo mengine na kusambaza kwa mitandao ya kijamii. Ni vyema ukaitumia mitandao hiyo ya kijamii kuleta watu kwenye blog yako.
- Shiriki kwenye majukwaa mengine mtandaoni na pia andika kwenye mitandao au blog nyingine kubwa. Licha ya kuwa na blog yako mwenyewe pamoja na mitandao ya kijamii, bado utakuwa unawafikia watu wachache wanaojua kuhusu wewe. Ili kuwafikia watu wapya, unahitaji kutumia mitandao mingine yenye wafuasi wengi. Mfano kuandika makala na kutuma kwenye blog maarufu au mitandao mikubwa, ambapo watu watasoma makala hizo na kukutafuta zaidi. Njia hii inafanya wazo lako lisambae na watu wakujue zaidi. Pia unaweza kutumia vyombo vya kawaida vya habari kama TV, redio na hata magazeti.
- Andika kitabu. Njia nyingine ya kuwafikia watu wengi kwa wazo lako ni kuandika kitabu ambacho kimedadavua wazo hilo vizuri. Kupitia kitabu hicho watu wanaweza kujifunza wazo lako jipya na jinsi ya kulitumia kuwa bora zaidi. Hii ndiyo njia ya uhakika kabisa ya kusambaza wazo lako. Lakini itakuwa na mafanikio kama utakuwa umeanza na njia hizo hapo juu. Mfano kama tayari una blog ambayo ina wasomaji, unapotoa kitabu hao ndiyo wanakuwa wateja wako wa kwanza. Kadhalika wale wanaokufuatilia kwenye mitandao ya kijamii.
Njia hizi zinakuwezesha kuwafikia watu wengi na wazo lako, zitumie zote vizuri.
Hatua ya tatu ni wengi kwa wengi.
Umeshawafikia watu wachache muhimu na kutengeneza mtandao mzuri, kisha ukawafikia watu wengi kwa kutengeneza mtandao mkubwa, sasa unapaswa kwenda hatua ya tatu, ambayo ni kutengeneza jumuia ya watu kwenye wazo lako. Hapa sasa wale watu wanaojua kuhusu wazo lako, wanalisambaza kwa wengi zaidi. Na hii ni hatua nzuri sana kufikia kwa sababu nguvu ya wengi wanaosambaza wazo lako inakusukuma kufanikiwa zaidi.
Katika kutengeneza jumuia ya watu wanaolizunguka wazo lako, zipo njia unazoweza kutumia kukuza zaidi jumuia hiyo.
- Kuwa mtu wa kati. Kupitia mtandao uliotengeneza, wajue watu wako vizuri, kisha ona ni watu gani ambao wakikutana watakuwa na manufaa kwa kila mmoja. Baada ya kuwajua watu hao, mweleze kila mmoja kuhusu mtu unayetaka kumkutanisha naye, jinsi ambavyo kukutana kwao kutawanufaisha wote. Wote wanapokubali kukutana, basi unawakutanisha na kuwaacha waendelee. Kwa njia hii watu watanufaika na watakuona wewe kama mtu ambaye umesababisha mafanikio yao na hivyo kukutangaza zaidi.
- Tengeneza jukwaa ambalo linawaleta pamoja watu ambao wanaamini kwenye wazo unalofanyia kazi. Jukwaa hili linakuwa sehemu ya watu kusaidiana, kubadilishana mawazo na hata kupeana uzoefu na fursa mbalimbali. Kadiri jukwaa unalotengeneza linavyokuwa imara, ndivyo waliopo kwenye jukwaa hilo wanawaleta wengine wengi zaidi.
- Tengeneza wafuasi kwenye wazo lako. Hapa wewe unakuwa kiongozi ambaye watu watapenda kukufuata kuhusiana na wazo lako. Hapa unaweka juhudi kwenye kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi kupitia wazo lako. Unapokuwa kiongozi na kujali kuhusu wengine, wafuasi wako wanakuletea watu wengi zaidi na hivyo wazo lako kusambaa zaidi.
- Fanya jukwaa lako kuwa sehemu ya furaha. Watu wengi wamekuwa hawapendi kujiunga na majukwaa au makundi mbalimbali kwa sababu yanakuwa na utaratibu mkali ambao unaonekana kuwabana sana watu. Sasa epuka hilo kwa kufanya jukwaa au kundi lako kuwa sehemu ya furaha, sehemu ambayo watu wanafurahia kuwepo. Sehemu ambayo watu wanasubiria kwa hamu kukutana, kwa sababu wanajua watajifunza, watafurahia na kupiga hatua zaidi.
Kwa njia hizi, utaweza kuwafanya wale ambao wanakubaliana na wazo lako kukuletea watu wengine wengi zaidi, na hapo wazo lako linakuwa linasambaa kwa kasi sana.
SEHEMU YA TATU; KUFIKIA MAFANIKIO MAKUBWA.
Umeshapata wazo la tofauti na la kipekee, ukaweka nguvu kwenye kutengeneza wafuasi wa wazo hilo na sasa wazo lako linakua na kusambaa kwa kasi ya ajabu. Hapa ndipo wengi hufanya makosa kwa kushindwa kuendeleza wazo lao na kufikia mafanikio makubwa. Lakini pia kwa hatua mbili zilizopita ulikuwa unajenga msingi zaidi, hivyo huenda ulikuwa hutengenezi kipato chochote au kama ulikuwa unatengeneza basi ni kidogo sana.
Sehemu hii ya tatu utajifunza jinsi ya kuendeleza wazo lako na kufikia mafanikio makubwa na pia jinsi ya kutengeneza kipato kikubwa kupitia wazo lako hilo.
Hapa nakwenda kukushirikisha hatua za kuchukua ili kuimarisha wazo lako na kufanikiwa sana. Kwenye makala ya #MAKINIKIA nitakushirikisha njia kumi za kutengeneza kipato kikubwa kupitia wazo lako.
Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia ili kuweza kuimarisha wazo lako na kufanikiwa zaidi.
Moja; tenga muda wa kutafakari.
Kutokana na wazo lako kusambaa kwa kasi, kila mtu atakuwa anataka muda wako. Kama usipokuwa makini, utajikuta muda wako mwingi unautumia kutimiza matakwa ya wengine na kujisahau wewe mwenyewe. Hivyo ili kuboresha wazo lako na hata kufanikiwa unahitaji kutenga muda wako wa kutafakari, muda ambao hutasumbuliwa na chochote au yeyote. Huu ni muda ambao utaendelea kujifunza zaidi na pia utatumia muda huo kuimarisha wazo lako zaidi, kadiri unavyojifunza na kupokea maoni ya wale anaofanyia kazi wazo hilo.
Mbili; tengeneza muda wa bahati.
Kadiri unavyofanikiwa, ndivyo muda wako unavyozidi kuugawa kwenye vitu vingine, hivyo ni rahisi sana kujisahau wewe mwenyewe. Unaweza kujikuta siku yako nzima umeipangilia, ni vikao, kazi, mikutano na kadhalika. Kwa ratiba iliyobana kama hii huwezi kupata muda wa kuruhusu akili yako kuja na ubunifu wa tofauti. Hivyo unapopanga ratiba yako ua siku, acha muda ambao hujaupangia chochote, huu ni muda ambao akili yako itazurura itakavyo. Katika hali hii ya kuzurura kwa akili, ndiyo unakutana na mawazo mapya na mazuri ambayo wengi huita bahati. Wakati mwingine tumia muda ambao upo barabarani au unasubiri kitu, badala ya kukimbilia kushika simu au kusoma kitu, iache akili yako izurure na utaweza kupata mtazamo wa tofauti.
Tatu; weka juhudi kubwa.
Watu wanapopata wazo moja la tofauti na wakaona limekubalika na wengi huwa wanajisahau, huwa wanaona wameshafanikiwa na hivyo hawahitaji tena kujisumbua. Na hapo ndipo wengi wanapoanza kuanguka. Kama unataka kufikia mafanikio makubwa, unahitaji kuendelea kuweka juhudi kubwa kwenye wazo ulilonalo sasa na hata kuja na mawazo mapya. Kila hatua ambayo umechukua, unahitaji kurudia na kuiboresha zaidi. Mfano unahitaji kuendelea kukuza blogu yako, kuwafikia wengi zaidi kupitia mitandao ya kijamii, kuendelea kuandika vitabu zaidi na hata kutengeneza wafuasi na kuwawezesha kupiga hatua zaidi. Juhudi zako hizi zitakufanya ubaki kwenye kilele cha mafanikio mara zote. Usifike mahali na kuona umeshafanikia na huhitaji kuweka juhudi tena, juhudi zaidi zinahitajika.
Rafiki, hivi ndivyo unavyoweza kupata wazo jipya na la tofauti, kutengeneza wafuasi kwenye wazo hilo na kuweza kufanikiwa zaidi. Fanyia kazi hatua hizi tatu na yale yaliyo ndani ya kila hatua na utaweza kufanikiwa sana kwenye chochote unachofanya.
Usikose #MAKINIKIA ya juma hili ili ujifunze njia kumi za kutengeneza kipato kikubwa kupitia wazo lako bora ulilotengeneza. Utaratibu wa kupata makinikia upo mwisho wa makala hii.
#3 MAKALA YA JUMA; HATUA SITA ZA KUFIKIA UBOBEZI.
Njia pekee ya kujitofautisha na wengine kwenye kile tunachofanya ni kwa sisi kubobea sana kwenye kile ambacho tunafanya.
Tunapaswa kubobea kiasi kwamba mtu anapokuwa na uhitaji wa kile tunachofanya, anatufikiria sisi pekee.
Lakini watu wengi wamekuwa hawajui ni njia ipi sahihi ya kufikia ubobezi. Wengi wamekuwa wanajaribu kufanya vitu vingi na kushindwa vibaya.
Wengi pia wamejaribu kitu kimoja lakini hawaweki juhudi za kuweza kuwafikisha kwenye ubobezi.
Kwenye makala ya juma hili, tumejifunza hatua sita za kufikia ubobezi kwenye chochote kile ambacho mtu unakifanya.
Kwa kufuata hatua hizi sita, kila mtu anaweza kutengeneza ubobezi mkubwa kwenye kile anachofanya na hata kutumia ubobezi huo kwenye mambo mengine pia.
Kama hukupata nafasi ya kuisoma makala ya juma hili, unaweza kuisoma sasa hivi hapa; Hatua Sita (06) Za Kutengeneza Ubobezi Kwenye Kile Unachopenda, Kutoa Thamani Zaidi Na Kuongeza Kipato Chako.
Pia endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku ili kujifunza, kuhamasika na kuchukua hatua na maisha yako yaweze kuwa bora zaidi.
#4 TUONGEE PESA; USIOGOPE KUWAAMBIA WATU WAKULIPE.
Watu wengi wanaofanya biashara za huduma, hasa za ushauri au mafunzo, huwa wanaanza kutoa huduma hizo bure ili watu wawajue. Ni vigumu sana kuanza kwa kuwachaji watu fedha ndiyo uwashauri au kuwafundisha mambo mbalimbali.
Hivyo mtu anapoanza kutoa huduma zake bure, watu wengi wanamfuatilia na kujifunza au kunufaika na huduma hizo kama ni za ushauri au nyinginezo.
Sasa mtu anaweka juhudi kubwa kutengeneza wafuasi wengi, akiwa na lengo kwamba watu wanaomfuatilia wanapokuwa wengi na wengi zaidi kuhitaji huduma zake, basi anaweza kuwatoza ada na kutengeneza kipato.
Lakini unapofika wakati wa kuwaambia watu wakulipe ili kuendelea kupata huduma ambazo umekuwa unawapa bure, wengi huwa wanaogopa. Wengi wanajenga hofu hii pale wanapoanza kuwaambia watu kuhusu malipo na watu hao wakawaambia hawakutegemea kulipia ushauri au mafunzo yanayotolewa.
Watu wengi ambao wamekuwa wananufaika na mafunzo hayo ya bure watapinga sana pale mtu aliyekua anatoa mafunzo hayo bure anapoanza kutoza ada. Na hili limekuwa linawafanya wengi kushindwa kuendelea na huduma zao na hivyo huduma hizo zinakufa.
Nikuambie leo rafiki yangu, kama unaendesha huduma yoyote ile, iwe ni ushauri, uandishi, ukocha, au huduma ya kiimani, lazima ujue kwamba ili huduma hiyo iendelee unahitaji njia ya kukuingizia kipato. Hivyo basi usiogope kuwatoza watu fedha pale wanapohitaji huduma zaidi kutoka kwako.
Nikitumia mfano wa AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA, nilianza kuandika kwenye AMKA MTANZANIA bure kabisa na mpaka leo mafunzo ya AMKA MTANZANIA ni bure kabisa. Baadaye nikaanzisha huduma ya KISIMA CHA MAARIFA ambayo ili mtu apate mafunzo yake, ni lazima alipe ada. Watu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba kama lengo ni kuwasaidia watu kwa nini natoza ada. Na huwa nasema wazi, isingekuwa ni kwa watu wachache wanaolipia huduma ya KISIMA CHA MAARIFA basi hayo mafunzo ya AMKA MTANZANIA yanayopatikana bure kabisa yasingekuwepo. Kwa sababu kuendesha mtandao huo wa AMKA MTANZANIA kuna gharama zake. Hivyo kinachoniwezesha niweze kuwasaidia wengi zaidi kwa mafunzo ya bure ninayotoa, ni wale wachache wanaolipia mafunzo mengine ninayotoa.
Hivyo rafiki, huduma yoyote unayotoa kwa wengine, kama ina thamani kwao, kama inayafanya maisha yao kuwa bora basi usiogope kuwaambia wakulipe. Wale wenye kuelewa na wanaonufaika kweli watakulipa na wale ambao hawaelewi watalalamika. Wewe kazana na wanaoelewa na kunufaika, kwa sababu huwezi kumridhisha kila mtu.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; NJIA PEKEE YA KUJIHAKIKISHA USALAMA KWENYE KAZI AU BIASHARA YAKO.
“In today’s competitive economy, it’s not enough to simply do your job well. Developing a reputation as an expert in your field attracts people who want to hire you, do business with you and your company, and spread your ideas. It’s the ultimate form of career insurance.” ― Dorie Clark
Wakati mapinduzi ya viwanda yanaanza, watu waliambiwa ili kuwa na usalama wa kazi basi soma kwa bidii, faulu sana na utapata kazi nzuri ambayo utaifanya mpaka kustaafu kwako na hapo utalipwa mafao ya kukuwezesha kuishi mpaka uzeeni.
Mapinduzi ya viwanda yamefika tamati na sasa tupo kwenye mapinduzi ya taarifa. Katika zama hizi uhakika pekee wa wewe kuwa na usalama kwenye kazi au biashara siyo tu elimu au taaluma uliyonayo, bali kutengeneza ubobezi kwenye kile unachofanya kiasi kwamba watu watapenda kufanya kazi na wewe.
Unapaswa kujijengea sifa ya ubobezi wa hali ya juu kwenye kile unachofanya kiasi kwamba kila mwenye uhitaji unaohusu unachofanya anakufikiria wewe au anaambiwa waje kwako.
Na hilo linawezekana kama utaweka juhudi katika kujua vizuri kile unachofanya, kukifanya vizuri na pia kutengeneza mtandao wa watu wanaojua kuhusu unachofanya na hivyo kusambaza sifa zako kwa wengine wengi.
Rafiki, hizi ndizo tano za juma hili la 28, tano ambazo zimelenga zaidi kwenye ubobezi ambao kila mmoja wetu anauhitaji ili kupiga hatua zaidi kwenye maisha yake.
Kwenye #MAKINIKIA tunakwenda kujifunza NJIA KUMI ZA KUINGIZA KIPATO kupitia kile ambacho unapenda kufanya na ambacho umejenga ubobezi kwenye kukufanya. Kwa sababu kama tulivyoona unahitaji ubobezi, lakini pia unahitaji kuendesha maisha yako. Zipo njia kumi ambazo mtu yeyote anaweza kutengeneza kipato kizuri kupitia ubobezi aliojijengea, kwenye #MAKINIKIA tutajifunza hayo. Usikose kabisa #MAKINIKIA ya juma hili, yatakupa mwanga mkubwa kwa upande wa kuongeza kipato chako.
#MAKINIKIA yanapatikana kwenye channel yetu ya telegram ya TANO ZA JUMA. Kama bado hujajiunga na channel hii basi jiunge sasa kwa maelezo ambayo yako hapo chini.
#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.
Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.
Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.
Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu