Kosa kubwa tunalofanya kwenye maisha yetu na mwenendo wetu wa kila siku ni kujifikiria zaidi sisi wenyewe kuliko wengine.
Kwa mfano wewe ukiwa unaumwa na kichwa unataka kila mtu aelewe ni maumivu kiasi gani unayapata.
Lakini mtu mwingine anapokuambia anaumwa na kichwa ni rahisi kumwambia ajikaze au avumilie, hasa pale anapokuwa ana kitu muhimu unataka akamilishe kufanya.
Wengine huweza kwenda mbali zaidi na kufikiri huenda mtu haumwi na kichwa kweli, anasingizia tu kwa sababu anajua hakuna anayeweza kupima maumivu ya kichwa ya mtu mwingine.
Sasa hili pia linakuja kwenye siku zetu na namna tunavyoziendesha.
Kuna siku ambazo unakuwa na siku mbaya tu, siku haiendi kama ulivyopanga, kitu ambacho ni rahisi kupata msongo au kuvurugwa. Katika siku za aina hii, huwa tunapenda sana watu watuelewe na watuache, wasitusumbue.
Lakini huwa tunasahau kwamba watu wengine nao huwa wanakuwa na siku ambazo siyo nzuri kwao, siku ambazo mambo yao hayaendi kama walivyotarajia, siku ambazo wanatamani sana wengine wangewapa wepesi zaidi.
Hivyo ni wajibu wako kutambua pale wengine wanapokuwa na siku ambazo siyo nzuri kwao, ili kuwapa wepesi.
Usichukulie kila kitu anachofanya mtu kama amefanya kwa kusudi au dharau, wakati mwingine ni mtu ana siku mbaya.
Labda ni mtu umemsalimia na hakuitika, au amekupa huduma ambayo ni mbovu, au amekujibu kwa mkato. Kabla hujakimbilia kusema mtu huyo ana dharau au hajali, jaribu kujiuliza kama hayupo kwenye siku yake mbaya. Mpe tena nafasi nyingine siku nyingine na hata nyingine tena. Utajifunza kwamba watu wengi ni wema na wanajitahidi kufanya kilicho bora, lakini hali fulani wanazopitia ndiyo zinawakwamisha.
Kwa upande mwingine sasa, japokuwa kila mtu anakuwa na siku zake mbaya, kazana sana siku yako mbaya isipeleke athari kwa wengine. Hata kama una siku mbaya kiasi gani, hata kama umekwazika kiasi gani, unapopata nafasi ya kukutana na watu wengine, unapopata nafasi ya kuwahudumia watu wengine, sahau ubaya wa siku yako na weka akili, hisia na nguvu zako zote kwa wale wengine na utaweza kuwahudumia vizuri sana. Usikubali siku yako mbaya izalishe siku mbaya kwa wengine pia. Una nguvu ya kusimama imara licha ya uwepo wa changamoto za kila siku.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante Kwa kocha, ni kweli kila mtu ana siku yake mbaya. Umenena vema.
LikeLike
Karibu.
LikeLike