“Receive without pride, let go without attachment.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 8.33
Tumepata nafasi ya kuiona siku hii nyingine nzuri sana kwetu leo.
Ni nafasi ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUPOKEA NA KUTOA…
Huwa tunayaharibu maisha yetu kwa namna tunavyopokea na hata kutoa vitu tunavyokutana navyo kwenye maisha.
Tunajisahau sana na hilo linakuja kutuumiza sana baadaye.
Tatizo huwa linaanzia kwenye kupokea, pale tunapopokea tunakuwa na kiburi na ufahari. Kwa kuona kwamba sisi tunastahili sana ndiyo maana tumepata, kwa kuona nguvu na akili zetu ndiyo zimetufanya tupate tulichopata.
Tunasahau kabisa nafasi ya bahati na hata upendeleo ambayo tumekutana nayo kwenye maisha yetu.
Tatizo linakua zaidi pale unapofika wakati wa kutoa kile tulichopokea, iwe ni kwa kurudisha au kupoteza. Huwa hatukubali kabisa kuachana na kike tulichopata au kuwa nacho. Tunakuwa tumejishikiza nacho, tunakiona ni sehemu yetu. Hivyo kinaoondoka tunaumia na kulalamika.
Rafiki, kuepuka kuumia ishi kwa msingi huu; UKIPATA SHUKURU, UKITOA AU KUPOTEZA SHUKURU.
Kumbuka hakuna kitu chochote ambacho umekuja nacho hapa duniani, na hakuna kitu chochote ambacho utaweza kuondoka nacho.
Hivyo chochote ulichonacho sasa, chochote utakachokuwa nacho kwenye maisha yako, umepewa jukumu la kukishikilia kwa muda, utafika wakati ambapo utapaswa kukitoa kwa wengine.
Hivyo unapopokea usiwe na kiburi na unapotoa usiwe na malalamiko. Ishi kwa msingi huu na kila wakati utakuwa na maisha bora sana.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kushukuru pale unapopokea na kushukuru pale unapotoa au kupoteza.
#HakunaUnachomiliki #UlichonachoUnakisimamiaKwaMuda #ShukuruKwaKilaJambo
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1