“When you see someone often flashing their rank or position, or someone whose name is often bandied about in public, don’t be envious; such things are bought at the expense of life. . . . Some die on the first rungs of the ladder of success, others before they can reach the top, and the few that make it to the top of their ambition through a thousand indignities realize at the end it’s only for an inscription on their gravestone.”
—SENECA, ON THE BREVITY OF LIFE, 20

Ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu,
Leo tumeipata nafasi hii nyingine nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KABLA HUJAONA WIVU, JUA KUNA GHARAMA ZA KULIPA…
Ni rahisi kuwaangalia watu waliofanikiwa na kutamani sana kuwa kama wao.
Ni rahisi kuona wivu kwa maisha ya watu hao, kuona na wewe unastahili kupata kile ambacho watu hao wanacho.
Tunachosahau ni kwamba, kuna gharama kubwa sana ambazo watu hao wamelipa ili kufika pale walipofika.
Wapo ambao wamelipa gharama za kiafya, kwa kusahau afya zao na kukazana na mafanikio pekee.
Wapo ambao wamelipa gharama za mahusiano yao, kwa kuacha mahusiano yavurugike na kukazana na mafanikio,
Na wapo ambao wamelipa gharama za kijamii, kwa kuachana na jamii na yale wengine wanafanya na kukazana na mafanikio yao tu.

Kabla hujawaangalia wale waliofanikiwa na kutamani mafanikio yao, jua kwanza gharama zipi wamelipa na kisha jiulize je upo tayari kulipa gharama hizo.
Kisha kama ni gharama unazoweza kulipa, basi zilipe.
Wengi wamekuwa wanakosea sana inapokuja kwenye mafanikio, wanasikiliza hadithi ya upande mmoja, alitoka hapa(chini) akafika hapa(juu), lakini hawajisumbui kujua gharama ambazo mtu amelipa katikati ya safari.
Hakuna mtu aliyefanikiwa ambaye maisha yale ni ya kawaida, lazima utakutana na kitu ambacho hakipo sawa kwao.

Mtu mmoja mwenye mafanikio makubwa sana duniani, akiwa anahojiwa aliulizwa unafanya kazi kwa muda kiasi gani, akajibu masaa 120 kwa wiki (yaani zaidi ya masaa 17 kila siku). Watu wakaanza kumsema na kumshauri kwamba anachofanya siyo sahihi, anaharibu afya yake, anapuuza mahusiano yake n.k. Lakini yeye alichojibu ni kimoja, hiyo ndiyo njia pekee ya kuweza kupata matokeo makubwa, na hataacha kuitumia.

Hivi ndivyo unavyopaswa kusimama na wewe pia kama unataka mafanikio makubwa, kujua gharama kubwa unayopaswa kuilipa kwenye maisha yako binafsi na kisha kulipa gharama hiyo.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujua gharama ambazo watu wamelipa kwenye mafanikio yao kabla hujawaonea wivu.
#MafanikioMakubwaYanaGharamaKubwa #JuaUpandeWaPiliWaMafanikio #HakunaAliyefanikiwaAkabakiKawaida

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1