Karibu kila mtu analalamika kwamba hana muda.

Ukweli ni kwamba muda upo wa kutosha sana, ila ni namna gani tunatumia muda huo ndiyo inaleta tofauti kwenye maisha yetu.

Pale unapokuwa huna muda, maana yake kuna vitu vingi unavyotaka kufanya kuliko muda ambao upo. Hivyo unapojaribu kufanya vitu hivyo, ndiyo unagundua kwamba muda haukutoshi.

Hivyo basi, suluhisho la changamoto ya muda, njia pekee ya wewe kupata muda zaidi ni kuacha kufanya vitu. Ni rahisi, lakini ngumu kutekeleza.

Kila unapojiambia kwamba huna muda wa kufanya vitu muhimu, kaa chini na orodhesha vitu vyote ambavyo unafanya kwenye siku yako. Orodhesha kila unachofanya kwenye muda wako wa masaa 25.

Kisha pitia orodha hiyo, na kweli kila ulichoandika kwamba unafanya, jiulize je kitu hicho ni muhimu kabisa kwako, kinakuingizia kipato au kuyafanya maisha yako kuwa bora? Kama jibu ni ndiyo basi kinabaki, kama jibu ni hapana basi kinaondoka mara moja. Hapa utaondoa vitu vingi ambavyo umekuwa unafanya sasa, ambavyo havina umuhimu kabisa.

Ukishaondoa yale ambayo hayana manufaa kabisa, bado utabaki na mengi ya kufanya ambayo yana manufaa kiasi. Hapo sasa utaanza kupima manufaa ya kila unachofanya. Na hapa ndipo unapotumia kanuni ya 20/80 ambapo unaangalia katika mambo 10 unayofanya, ni yapi 2 ambayo yanaleta matokeo makubwa kuliko mengine 8. Hapo unakazana na hayo mawili na kuachana na mengine yote.

Zoezi hili ni gumu kwa sababu watu huwa hawapendi kuacha kufanya vitu ambavyo wameshazoea kufanya. Hivyo huendelea kufanya vitu siyo kwa sababu vina manufaa, ila kwa sababu tu wamekuwa wanafanya.

Pia unapaswa kujua kwamba kila unapopata kitu kipya unachotaka kufanya, lazima kuna kitu cha zamani unachopaswa kuacha kufanya. Hivyo usianze kitu kipya kabla hujaacha cha zamani, kila wakati utaona muda haukutoshi.

Ukiacha kufanya vitu visivyo na umuhimu mkubwa, utapata muda wa kutosha wa kufanya vitu vyenye umuhimu mkubwa kwenye maisha yako.

Kama changamoto yako ni huna muda, jibu ni rahisi kwako, acha kufanya baadhi ya vitu unavyofanya sasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha