Rafiki yangu mpendwa,

Unapokutana na mtu ambaye amefanikiwa kuliko wewe, basi jua kuna kitu anachojua na anakifanya ambacho wewe hukijui au hukifanyi.

Mafanikio makubwa huwa hayaji kama bahati au ajali, bali ni matokeo ya hatua za tofauti ambazo mtu anachukua kwenye maisha yake.

Ndiyo maana tunapaswa kujifunza kwa wale ambao wamefanikiwa kuliko sisi, kujua ni vitu gani wanafanya tofauti ili na sisi tuweze kuvifanya na kufanikiwa pia.

Ipo siri moja ya mafanikio ambayo mabilionea wengi wamekuwa wanaijua na kuifanyia kazi na wengi hawaijui au hawaifanyii kazi. Siri hiyo ni kujifunza kupitia usomaji wa vitabu.

TANGAZO LA UZINDUZI VITABU (2)

Kwenye makala ya leo, tunakwenda kuwaoa mabilionea wakubwa watano ambao mafanikio yao yanatokana na usomaji wa vitabu.

  1. Bill Gates, mmiliki wa Microsoft na tajiri namba 2 duniani.

Bill Gates ndiye mwanzilishi na mmiliki wa kampuni kubwa ya teknolojia duniani ambayo ni Microsoft. Kwa mujibu wa orodha ya Forbes 2019, Bill Gates ana utajiiri wa dola bilioni 96.5 sawa na shilingi trilioni 222 za Kitanzania.

Bill Gates amekuwa msomaji mzuri sana wa vitabu. Kila mwaka huwa anasoma vitabu siyo chini ya 50, na kushirikisha yale aliyojifunza kupitia mtandao wake anaouita GATES NOTES. Kila mwaka Bill Gates huwa anajipa likizo ya wiki mbili ambapo hujifungia na vitabu bora kabisa na kuvisoma kwa kina.

Gates anakiri kwamba usomaji wa vitabu umemwezesha kuja na mawazo bora na ya tofauti ambayo yamemwezesha kufikia mafanikio makubwa aliyonayo sasa.

  1. Warren Buffett, CEO wa Berkshire Hathaway na tajiri namba 3 duniani.

Warren Buffett ambaye ni mwanzilishi na mkurugenzi wa kampuni kubwa ya uwekezaji inayoitwa Berkshire Hathaway ni mmoja wa wawekezaji wenye mafanikio makubwa sana duniani. Kwa mujibu wa orodha ya Forbes 2019, Buffett ana utajiri wa dola bilioni 82.5 sawa na shilingi trilioni 190 za Kitanzania.

Warren Buffett anasema asilimia 80 ya muda wake huwa anautumia kusoma vitabu na ripoti za makampuni mbalimbali. Anasema ni kupitia usomaji huu ndiyo ameweza kugundua kampuni bora za kuwekeza kitu ambacho kimempa utajiri mkubwa.

Siku moja mwanafunzi alimuuliza swali Buffett, kwamba ili awe mwekezaji bora afanye nini, Buffett alichukua karatasi na kumwonesha, akamwambia soma karatasi kama hizi 500 kila siku. Buffett anaamini sana kwenye usomaji wa vitabu, licha ya uzee wake wa zaidi ya miaka 80, mpaka sasa anasoma sana.

SOMA; Hivi Ndivyo Elimu Ya Msingi Ya Fedha Ilivyobadili Maisha Ya Wengi, Na Inavyoweza Kubadili Maisha Yako Pia.

  1. Mark Zuckerberg, CEO wa Facebook, tajiri namba 8 duniani.

Mark Zuckerberg ni mwanzilishi na mkurugenzi wa kampuni ya mitandao mikubwa ya kijamii duniani, yaani Facebook, Instagram na Whatsapp. Kwa mujibu wa orodha ya Forbes 2019, Zuckerberg ana utajiri wa dola bilioni 62.3 sawa na shilingi trilioni 143 za Kitanzania.

Katika kuuanza mwaka mpya wa 2015, Zuckeberg alijiwekea lengo la kusoma vitabu viwili kila mwezi kwa mwaka mzima. Na kwa mwaka huo aliweza kusoma na kushirikisha vitabu 24. Anakiri kwamba usomaji umemwezesha kuvuka changamoto za kuendesha kampuni kubwa duniani huku akiwa kijana mwenye umri mdogo. Ni mmoja wa mabilionea wenye umri mdogo sana. Usomaji wa vitabu ni moja ya vitu ambavyo vimemwezesha kufanikiwa sana katika kukuza kampuni yake ya mitandao ya kijamii.

  1. Elon Musk, CEO wa Tesla na Space X.

Elon Musk ni mmoja wa watu wa tofauti sana anayeishi zama hizi, wengi wamekuwa wanafikiri siyo binadamu wa kawaida. Hii ni kwa sababu mambo anayofanya siyo ya kawaida kabisa. Kwanza ni mwanzilishi na mkurugenzi wa kampuni ya magari yanayotumia umeme (Tesla) lakini pia ni mkurugenzi wa kampuni inayofanya utafiti angani (Space X). Musk anasema lengo lake ni kuhakikisha wanadamu wanaweza kuishi kwenye sayari ya Mars na mpango kamili anao na anaufanyia kazi kwa sasa.

Kwa mujibu wa orodha ya Forbes 2019, Elon Musk ana utajiri wa dola bilioni 20 sawa na shilingi trilioni 46 za Kitanzania.

Elon Musk amekuwa anaamini sana kwenye usomaji wa vitabu. Wakati anatengeneza roketi ya kwenda angani, alipouliza aliwezaje kuja na tofauti alijibu kwamba alijifunza kwenye vitabu vya hadithi za kisayansi alivyosoma utotoni. Akiwa mtoto alikuwa anasoma vitabu viwili kwa siku na kuvimaliza. Mama yake alikuwa na wasiwasi kwamba atakuwa kipofu kwa namna alivyokuwa anatumia muda mwingi kusoma.

  1. Charlie Munger, mwenyekiti msaidizi wa Berkshire Hathaway

Charlie Munger ni mshirika wa karibu wa Warren Buffett, wawili hawa wamekuwa wanaendesha kampuni ya uwekezaji ya Berkshire Hathaway kwa zaidi ya miaka 40 sasa. Wote ni wasomaji wazuri na Munger amekuwa anasema wakiwa ofisini na Buffett, kila mtu anakuwa anasoma. Kwa mujibu wa orodha ya Forbes 2019, Munger ana utajiri wa dola bilioni 1.7 sawa na shilingi trilioni 4 za Kitanzania.

Charlie Munger anajulikana zaidi kwa mfumo wake wa kufikiri na kufanya maamuzi unaoitwa Mental Models. Mfumo huu unamwezesha mtu kufanya maamuzi sahihi na kutokuingiliwa na hisia. Ameweza kutengeneza mfumo huu kupitia usomaji wake wa vitabu vingi. Amekuwa anasoma kila aina ya vitabu, kuanzia historia, saikolojia, fizikia, uchumi na kadhalika.

Watoto wa Munger huwa wanasema baba yao ni kama kitabu chenye miguu, kwa sababu muda wake mwingi anautumia kusoma.

Munger ana miaka zaidi ya 90, lakini mpaka sasa bado anatumia muda wake mwingi kusoma vitabu.

SOMA; Mambo Haya Kumi (10) Usiyojua Kuhusu Fedha Ndiyo Yanakufanya Uendelee Kuwa Masikini.

  1. Mimi na wewe.

Mimi na wewe ni mabilionea wa siku zijazo. Na tutaweza kufikia ubilionea huo kama tutaweza kuiga siri hii kubwa ya mabilionea, kwa kuwa wasomaji wazuri na kufanyia kazi yale ambayo tunajifunza kwenye usomaji wa vitabu.

Kama upo tayari kufikia ubilionea kwa kupata maarifa sahihi na kuyafanyia kazi basi nakukaribisha sana tusafiri pamoja kwenye safari hii.

Nakukaribisha kwenye uzinduzi wa vitabu viwili muhimu sana kwa mafanikio yako.

Vitabu hivyo ni ELIMU YA MSINGI YA FEDHA na TANO ZA MAJUMA 50 YA MWAKA.

Uzinduzi wa vitabu hivi utafanyika jumamosi ya tarehe 03/08/2019 jijini Dar es salaam.

Kwenye siku hii ya uzinduzi tutashirikishana mengi sana kuhusu usomaji wa vitabu na jinsi unavyoweza kutumia maarifa unayojifunza kupiga hatua kwenye maisha yako.

Nitakushirikisha hadithi yangu ya jinsi usomaji wa vitabu ulivyoweza kuokoa maisha yangu, kutoka kwenye kufukuzwa chuo kikuu na kukosa kabisa tumaini la maisha mpaka kuweza kuanzisha biashara ya kuuza maarifa mtandaoni na kuwafikia watu wengi, yote hayo kupitia usomaji wa vitabu na kuchukua hatua.

Usikose nafasi hii ya kipekee, ambayo itayabadili sana maisha yako na miaka 10 ijayo, utaangalia nyuma na kusema siku ya tarehe 03/08/2019 ndipo maisha yako yalibadilika kabisa.

Kupata nafasi ya kushiriki uzinduzi huu wa vitabu, tuma majina yako na namba ya simu kwa ujumbe kwenda namba 0717396253

Mwisho wa kupata nafasi ya kushiriki uzinduzi huu ni kesho tarehe 31/07/2019, hivyo chukua hatua sasa ya kutuma majina na namba yako ya simu ili usikose nafasi hii.

Nina amini sana kwenye usomaji wa vitabu, nina ushahidi wa kutosha kwa nini usomaji wa vitabu ndiyo kitu pekee kinachoweza kukukwamua hapo ulipokwama sasa, karibu tukutane tarehe tatu nikupe ushahidi huo na jinsi ya kuufanyia kazi, na wewe mwenyewe uyaone maisha yako yakiwa yanabadilika kwa kasi kubwa.

Nikutakie kila la kheri, hakikisha kwa chochote unachofanya, basi kupata maarifa kupitia usomaji wa vitabu kinakuwa kipaumbele cha kwanza kwako. Na kama unataka kujifunza kwa kina na kupata hamasa ya kusoma vitabu zaidi, basi karibu tukutane tarehe o3/08/2019, nitumie majina na namba yako sasa kwenye namba 0717396253 na nitakupa maelekezo zaidi.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge