Watu huwa hawapendi mtu apate kile kitu ambacho wao hawana.

Hasa watu wa karibu au ambao mpo ngazi sawa, kwa sababu wewe ukipata kitu ambacho wao hawana, hilo litawafanya wao waonekane ni wazembe.

Hivyo kama watu hawana fedha na utajiri, kwa hakika hawatataka wewe uwe na fedha na utajiri, kwa sababu hilo litawafanya waonekane wao ni wazembe. Watatafuta kila njia ya kukukwamisha ili kuhakikisha hupati fedha na utajiri.

Kama watu hawana furaha kwenye maisha yao hawatataka wewe uwe na furaha. Watakuwa mabalozi wazuri wa kukuhubiria habari mbaya na hasi ili kuhakikisha huwi na furaha.

Ili uwe na maisha bora na unayoyataka, hatua ya kwanza kwako ni kuwa makini na wale wanaokuzunguka. Jua ni vitu gani watu hao hawana lakini wewe ungependa kuwa navyo. Ukishajua vitu hivyo, basi kuwa makini sana nao watu hao kwenye ushauri au maoni wanayokupa kwenye vitu hivyo.

Mfano kama lengo lako ni kufikia uhuru wa kifedha, na wanaokuzunguka hawana uhuru wa kifedha, chochote wanachokuambia kuhusu fedha kuwa makini nacho, kwa sehemu kubwa hakitakuwa sahihi, na kuna nafasi ya wao kuwa wameongeza mambo mengine ili kukukwamisha.

Wakati mwingine watu wanafanya hivyo kwa kujua, wakati mwingine kwa kutokujua. Ni wajibu wako wewe kujua kipi cha kusikiliza na kubeba na kipi cha kuacha.

Kuwa makini sana na ushauri unaopokea kwa watu ambao hawana au hawafanyi kile wanachokushauri.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha