Kama una kitu ambacho unauza, au unafanya, au unajua na una uhakika na kuamini kwa asilimia 100 kwamba kitu hicho kina msaada kwa wengine, kinaweza kuwatoa pale walipo sasa na kuwapeleka mbali zaidi, basi ni jukumu lako kuwashawishi watu hapo mpaka wakubaliane na wewe kwenye kitu hicho.
Japokuwa watu watakuwa wabishi, watakataa, watakupinga na kukukwepa, lakini jua ni jukumu lako kuhakikisha watu hao wanapata kitu hicho.
Na kama utashindwa kuwashawishi watu kwenye kile kitu ambacho unaamini kweli kitawasaidia, basi wewe ni mbinafsi.
Hebu fikiria, kuna mtu ambaye ana maumivu makali sana, halafu wewe una dawa ya maumivu, lakini unashindwa kumweleza kwa namna ambayo ataelewa na apate dawa hiyo, huoni huo ni ubinafsi?
Kwamba wewe una kitu ambacho kinaweza kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora kabisa, lakini huchukui juhudi kuhakikisha wanakuelewa na kupata kitu hicho. Unaweza kujiambia watu hawataki wenyewe, au hawakuelewi na hivyo kuona siyo tatizo lako.
Lakini mimi nakuambia leo, hilo ni tatizo lako, na lazima uchukue hatua kuhakikisha unavuka hali hiyo.
Chukua mfano una mtoto mdogo, ambaye anakataa kula chakula kila siku. Je utajiambia hataki mwenyewe kwa hiyo naachana naye? Jibu ni hapana, utatafuta kila njia kuhakikisha anakula chakula, kwa sababu ndiyo uhai wake.
Hivyo sasa ndivyo unavyopaswa kuwachukulia wateja wako au watu unaowahudumia na kuwalenga, kama watoto ambao wewe umepewa jukumu la kuwalea, na hivyo unapaswa kuhakikisha wanapata kile kilicho bora.
Na ujue ya kwamba, kama hutaweka juhudi kuwashawishi wateja wako wakubaliane na wewe, ambaye una kitu sahihi kwao, kuna mtu mwingine atakuja, ambaye hana kitu bora kama ulichonacho wewe, akawashawishi na wakakubaliana naye. Sasa huoni kwamba wewe ndiye umewapeleka kwa mtu huyo asiye sahihi kwa kushindwa kuwashawishi?
Jitwike jukumu la kufanya maisha ya wateja na wale unaowahudumia kuwa lako, kuwa na bidhaa au huduma ambayo unaiamini kweli, na hakikisha kila ambaye inaweza kumsaidia basi anaijua na kuchukua hatua. Usipofanya hivyo basi jua wewe ni mbinafsi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,