Fikiria siku ambayo umeamka, kuweka mipango yako ya siku na kila kitu ulichopanga kikaenda kama ulivyokuwa umepanga, bila ya changamoto au kukwama popote. Halafu hivyo ndivyo kila siku yako inavyokuwa.

Amka kutoka usingizini, hizo ni siku ambazo zinakuwa kwenye ndoto. Kwenye uhalisia wa kawaida siku za aina hiyo hazipo. Kwenye uhalisia hakuna siku iliyokamilika, na kama zipo basi ni chache sana.

Utaweka mipango yako vizuri sana, utafanya kila unachopaswa kufanya, lakini kitatokea kitu ambacho kitakwenda tofauti au kuvuruga kila ambacho umeshafanya kwenye siku yako hiyo.

Je hili linatufundisha tusihangaike kupangilia siku zetu? hapana, hiyo itakuwa ni kukata tamaa.

Kitu ambacho hili linatufundisha ni kuweka mategemeo yetu kwa usahihi, kuacha kujidanganya kwamba siku ya mafanikio ni ile siku ambayo kila kitu kimekwenda kama tulivyopanga. Bali siku ya mafanikio ni siku ambayo tumeweza kufanya kadiri ya ubora wetu, siku ambayo tumeweza kujisukuma na kuwa bora zaidi.

Siku iliyokamilika siyo ile siku ambayo kila kitu kimeenda kama ulivyopanga, bali ni ile siku ambayo umekazana kufanya kile kilicho sahihi, kukazana kufanya kwa ubora na kutumia muda wako kwa yale muhimu pekee.

Kila mmoja wetu anaweza kuwa na siku iliyokamilika, ni kuamua namna gani tunatumia siku zetu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha