Mtu mmoja amewahi kunukuliwa akisema kama una jukumu muhimu ambalo unataka lifanyike, basi tafuta mtu aliyetingwa (aliye bize) na mpe jukumu hiyo afanye. Ukimpa mtu aliyetingwa jukumu analitekeleza kwa haraka, ukimpa mtu ambaye hajatingwa, ambaye ana muda mwingi, jukumu hilo litachelewa kutekelezwa.
Unaweza kuona iweje mtu ambaye tayari ametingwa ndiyo aweze kutekeleza jukumu huku ambaye hajatingwa ashindwe! Lakini ndivyo hali ilivyo, ndiyo maana waswahili walisema penye miti hapana wajenzi, labda ni kwa sababu waliopo kwenye miti hiyo wanafurahia vivuli vya miti na hivyo hawapati msukumo wa kujenga.
Ukweli ni kwamba, wingi wa rasilimali ni kikwazo kwa mafanikio yako, hasa pale unapoanza.
Ukiwachukua watu wawili wanaoanza safari yao ya mafanikio, mmoja akawa na rasilimali nyingi na mwingine rasilimali kidogo, mwenye rasilimali kidogo atafanikiwa haraka kuliko kwenye rasilimali nyingi.
Hii ni kwa sababu mtu anapokuwa na rasilimali nyingi anazitumia hovyo kwanza, ni mpaka pale zinapopungua kabisa ndiyo akili inamkaa sawa na kuzitumia vizuri. Lakini anayeanza na rasilimali kidogo anazitumia kwa umakini sana rasilimali hizo kwa sababu anajua akipoteza hana tena pa kuanzia.
Kama unaanza ukiwa na fedha nyingi, utakuwa na matumizi mengi ya fedha, ambayo mengi siyo muhimu, na hivyo nyingi utazipoteza. Lakini kama utaanza ukiwa na uhaba wa fedha, utapunguza sana matumizi yako na hivyo utahangaika na yale muhimu pekee. Kwa kuhangaika na yaliyo muhimu utaweza kupiga hatua zaidi.
Kama unaanza ukiwa na muda mwingi, utajikuta unapoteza sehemu kubwa ya muda huo, kwa kujaribu vitu visivyokuwa muhimu. Lakini kama una uhaba wa muda, utatumia muda huo kwa yale muhimu pekee.
Kama unaanza ukiwa na elimu kubwa, elimu hiyo itakupa woga wa kujaribu hatua kubwa, kwa sababu unakuwa na uelewa mpana sana wa ndani kwenye kile unachofanya. Lakini anayeanza bila ya elimu kubwa, hana kinachomzuia, anaweza kuwa na ndoto ambazo zinaenda kinyume kabisa na yale ambayo wenye elimu wamefundishwa na akazifikia kwa sababu hajapewa ukomo.
Rafiki, ni kweli kwa kila mmoja wetu, na kama ilivyo kwenye asili, kwamba uwepo wa rasilimali nyingi ni kikwazo kwa mafanikio. Angalia hata kwenye mataifa, yale yenye rasilimali nyingi hayana maendeleo makubwa kama yenye rasilimali kidogo.
Sasa unafanya nini hapa?
Ili kupiga hatua kwenye maisha yako, ili kufanikiwa zaidi, jitengenezee ukomo kwenye rasilimali ulizonazo. Hata kama una rasilimali nyingi kiasi gani, jiwekee ukomo kwa kutumia chache au kiasi kidogo.
Mfano, moja ya vitu vinavyowaangusha wengi wanaoanza biashara ni kutumia fedha zao vibaya. Sasa wewe panga kuingia kwenye biashara kwa nusu ya fedha ulizonazo na nusu inayobaki iweke kwenye gereza ambalo huwezi kutoa. Pambana na nusu hiyo kwa angalau mwaka mmoja na utaona jinsi utakavyopiga hatua zaidi.
Kadhalika kwa upande wa muda, jipe muda mfupi wa kufanya mambo na jisukume kutumia muda huo bila ya kuongeza. Kadiri muda wako unavyokuwa mchache ndivyo unaachana na yasiyo muhimu na kukazana kufanya yaliyo muhimu zaidi.
Usikubali wingi wa rasilimali uwe kikwazo kwa mafanikio yako, jiwekee ukomo wa rasilimali ulizonazo ili ukusukume kuwe na matumizi sahihi ya rasilimali hizo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha, nitaendelea kuweka Juhudi kwa kutumia rasilimali nilizonazo ili kuongeza kipato changu.
LikeLike
Vizuri Beatus,
Kila la kheri.
LikeLike
Asante kocha, huu ni ukweli mtupu
Kuwa na rasilimali nyingi ni kikwazo kufanikiwa. Asante Kwa hatua hizi za kuchukua ulizoshauri mtu achukue.
LikeLike
Vizuri Tumaini
LikeLike
Hakika kocha rasilimali nyingi ni kikwazo kufanikiwa, asante Kwa kutushirikisha hili.
LikeLike