Kazi ya kwanza uliyonayo kwenye maisha yako ni kujiuza wewe mwenyewe. Simaanishi kujiuza kama ilivyozoeleka kwa wale wanaotumia miili yao kibiashara. Bali namaanisha kujiuza kwa kuwashawishi wengine kukubaliana na wewe, kukupokea wewe na kushirikiana na wewe kwenye kile unachotaka kushirikiana nao.

Kama unatafuta kazi ya kuajiriwa lazima uweze kujiuza kwa mwajiri wako, akubaliane na wewe, awaache wengine wenye sifa na kukuajiri wewe. Na hata baada ya kuajiriwa, mauzo yanaendelea, unapaswa kumshawishi mwajiri wako kwamba kuendelea na wewe ni manufaa makubwa kwake. Kwamba kama kuna kosa anaweza kulifanya kwenye maisha yake basi ni kukupoteza wewe.

Kadhalika kwenye kujiajiri na kufanya biashara, unahitaji sana kujiuza kwa wateja wako, waache kununua kwa wengine wanaouza kile unachouza na waje kununua kwako. Na hata wanaponunua mara moja, wawe tayari kurudi kununua tena na tena na kuwaleta wengine nao wanunue pia.

Wote tunajua jinsi ambavyo dunia ya sasa imejaa kila aina ya kelele, kila mtu anaweza kuahidi mambo chungu mzima, na asiweze kutekeleza. Hata wateja wameshajifunza kwamba wengi wanaoahidi vitu hawawezi kuvitekeleza.

Sasa unawezaje kusimama na kuwashawishi watu wakubaliane na wewe. Zipo njia nyingi, lakini moja ambayo ina nguvu sana ukiifanyia kazi ni NENO MOJA.

Unapaswa kuwa na neno moja linalokuelezea wewe, neno moja ambalo likitamkwa basi wateja wanakufikiria wewe. Neno moja ambalo unaweza kumwahidi mteja na ukalitimiza kwa viwango ambavyo mteja hakutegemea.

Kwa kutengeneza neno moja linalokubeba, wateja watakwenda na wewe na pia itakuwa rahisi kwao kuwaambia na kuwaleta wengine pia.

Yapo maneno mengi sana, kazi ni kwako kuchagua lile ambalo litakuwezesha kusimama na kukutambulisha kwa wengine.

Kama umeajiriwa, neno lako moja linaweza kuwa; MCHAPAKAZI, MWAMINIFU, ANAYETEGEMEKA, ASIYEKATATAMAA.

Kama umejiajiri au unafanya biashara, neno lako moja linaweza kuwa; MWAMINIFU, THAMANI, MPAMBANAJI, MBEBAMAONO.

Yapo maneno mengine mengi kwenye maeneo tofauti, wewe chagua neno lako moja, kisha liishi neno hilo kwenye kila unachofanya, usiku na mchana, iwe unaonekana au huonekani.

Ukiweza kujijengea neno moja unalojulikana kwalo, kujiuza itakuwa rahisi kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha