Jukumu kubwa ambalo nimejipa kwenye maisha yangu, ni kuhakikisha wewe rafiki yangu, wewe ambaye umejiunga na mafunzo mbalimbali ninayotoa, unapata fedha zaidi.

Ndiyo maana nimekuwa nakushirikisha mafunzo mengi yenye maarifa sahihi kuhusu fedha, na hata kukupa hatua za kuchukua ili kuongeza kipato chako zaidi.

Na leo nakurudisha kwenye msingi muhimu sana kuhusu fedha, msingi ambao kila mmoja wetu anapaswa kuujua na kuuishi ili kupata fedha zaidi.

Msingi huu unaanzia kwenye fikra tulizonazo kuhusu fedha.

Kwa jamii tulizokulia na wale waliotuzunguka, imani ni kwamba kuna uhaba wa fedha, kwamba wote hatuwezi kuwa matajiri, kwamba wachache tu ndiyo wanaoweza kupata fedha na kutajirika.

Leo nakuambia huo ni uongo, hicho kitu hakipo, ni imani tu potofu, lakini siyo uhalisia.

Hakuna uhaba wa fedha hapa duniani, kwa kifupi hakuna uhaba wa kitu chochote hapa duniani. Hebu fikiri kwa miaka yote ambayo binadamu tumekuwa tunakula samaki, lakini samaki hawaishi, kwa sababu kila siku wanazaliwa, tena wengi mno.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye fedha. Hakuna uhaba wa fedha, kila siku zinazalishwa fedha nyingi mno. Kila siku zipo fursa za kutengeneza fedha zaidi, kupitia chochote ambacho mtu anafanya.

Hebu angalia watu wanaokuzunguka hapo ulipo sasa, halafu niambie kama hawali, hawavai, hawasafiri, hawafanyi sherehe mbalimbali, hawajengi, hawapeleki watoto shule na kadhalika?

Unafikiri vitu hivyo wanavifanya kwa kutumia nini? Jibu lipo wazi, wanafanya vyote hivyo kwa kutumia fedha, sasa kwa kuwa watu wanaongezeka kila wakati, ni dhahiri fedha zinaongezeka pia.

Ondoka kwenye mtazamo wa uhaba inapokuja kwenye fedha na nenda kwenye mtazamo wa utele. Hakuna uhaba wa fedha, fedha zipo za kutosha kama tu utakuwa tayari kutoa thamani ambayo watu wanaihitaji na wapo tayari kutoa fedha zao ili wapate thamani hiyo.

Nenda kakusanye fedha zako rafiki, zipo nyingi na zinakusubiri, ni wewe tu uchukue hatua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha