Rafiki, je umewahi kujikuta njia panda, ambapo unakuwa hujui useme nini au ufanye nini? Hii ni hali ambayo huwa inatukuta mara nyingi kwenye kazi zetu na hata maisha yetu pia. Tunakwama kuchukua hatua kwa sababu hatujui kipi tufanye. Au tunashindwa kutoa majibu kwa sababu hatujui nini tuseme.

Sasa unajua wazi kabisa ya kwamba kutokuchukua hatua ndiyo kikwazo kikubwa kwa wengi kutokufanikiwa, hivyo unapaswa kuchukua hatua pale unapopaswa kufanya hivyo. Lakini sasa upo njia panda, hujui ni hatua ipi uchukue au useme nini.

Kwenye makala ya leo, tunakwenda kujifunza kitu cha kufanya au kusema pale unapokuwa njia panda.

Tukianza na kufanya, mara zote fanya kile kilicho sahihi. Unapojikuta njia panda, ukiwa na vitu vingi vya kufanya na hujui kipi cha kufanya, basi fanya kile kilicho sahihi. Hicho pekee ndiyo kitakachokusaidia. Najua hapa unaweza kukwama tena, kwa kutokujua kilicho sahihi ni kipi. Na hilo pia lisikukwamishe, kama hujui kipi sahihi kufanya, basi anza kwa kufanya chochote. Ni bora kukosea kwa kufanya kitu, kuliko kukaa bila kufanya kitu kabisa. Kwa sababu unapofanya na ukakosea, unajifunza na hapo utajua kipi sahihi na bora kufanya. Usikubali kukwama na kutokuwa na cha kufanya kabisa, anza kwa kufanya kilicho sahihi na kama hujui kilicho sahihi basi fanya chochote.

Tukienda kwenye kusema, unapokuwa njia panda na hujui useme nini, basi sema ukweli. Mara zote sema ukweli, hata kama unaumiza kiasi gani, ni ukweli pekee utakaokuweka huru, utakaokuepusha na matatizo makubwa zaidi baadaye. Najua hapa pia unaweza kukwama, kwa kuwa hujui ukweli ni upi, na hapo sasa hatua sahihi ya kuchukua ni kukaa kimya. Kama hujui ukweli ni upo, usikimbilie kusema chochote, badala yake kaa kimya. Na kukaa kimya hakujawahi kumuumiza yeyote, bali kusema hivyo kumewaweka wengi kwenye matata.

Kama utakuwa umeona hapo, kama hujui kilicho sahihi kufanya unaweza kufanya chochote, kwa sababu hata ukikosea, unaweza kuchukua hatua bora zaidi na ukarekebisha chochote ulichoharibu. Lakini kama hujui kipi sahihi na kweli kusema, unapaswa kukaa kimya, kwa sababu maneno ukishayatoa, hakuna namna ya kuyarekebisha. Usikimbilie kuongea chochote pale unapokuwa hujui kilicho kweli au sahihi kusema, kaa kimya. Ukishayatoa maneno, hayarudi tena, na huwezi kuyarekebisha kwa maneno mengine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha