Kuna mambo mengi tumekuwa tunafanya kwenye maisha yetu, ambayo siyo tu hayana manufaa, lakini pia yanapoteza muda wetu kwa kuvuruga utulivu wa ndani yetu.
Mfano kuna mahali unakwenda, na unataka sana kuwahi, lakini njiani ukakutana na foleni ambayo ni ndefu na inakwenda taratibu sana. Hapo unaanza kupatwa na mawazo mengi, kwamba utafika saa ngapi, je utawahi au kuchelewa na mengine kama hayo.
Lakini wasiwasi wowote unaokuwa nao katika hali hiyo, hauna msaada kabisa, kwa sababu huna njia ya kuharakisha foleni hiyo, ni kitu ambacho kipo nje ya uwezo wako.
Na kuhusu utafika saa ngapi, huwezi kutabiri hilo kwa uhakika, ila kuna kitu kimoja una uhakika nacho, kwamba utafika utakapokuwa umefika.
Sijui kama unaielewa vizuri hivyo dhana, kwamba badala ya kujisumbua sasa kwa kujiuliza utafika saa ngapi, wewe jiambie utafika pale utakapofika. Na hivyo basi, kwa sasa, badala ya kujisumbua kujiuliza utafika saa ngapi, peleka mawazo yako kwenye kutafakari mambo mengine muhimu, kwa sababu utafika utakapofika. Yaani ukishafika kule unakokwenda, ndiyo unakuwa umefika, kwa sasa siyo kitu cha kukupa mawazo wala wasiwasi.
Njia nyingine ya kuchukulia hili ni dhana ya kuvuka daraja. Ambapo huwa tunaambiwa, unavuka daraja utakapolifikia. Kama una safari ambayo inakuhusisha kuvuka daraja, haijalishi unafikiria kiasi gani kuhusu daraja hilo unapokuwa unaianza safari yako, hilo halitakusaidia kwenye kuvuka daraja hilo. Unapofika kwenye daraja ndiyo unapata fursa ya kulivuka.
Kama utaweza kutumia dhana hizi kwenye kila unachofanya, utaondokana na hofu na wasiwasi na kuwa na utulivu mkubwa sana ndani yako. Hata kama mambo hayaendi kama ulivyopanga, unajua kila kinachotokea kina manufaa kwako na hivyo huumii wala kupoteza muda wako kwa mambo yasiyo na maana. Unatumia kila hali unayokutana nayo au kupitia kama unavyokuja kwako na unaitumia kwa ubora zaidi.
Utafika utakapofika na utavuka daraja utakapolifikia, lakini kwa sasa, kuwa na utulivu na fanya kile unachokifanya kwa ubora wa hali ya juu kabisa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ni kweli fanya unalofanya sasa Kwa utulivu utavuka daraja utakapolifikia
LikeLike
Hakika.
LikeLike