Watu huwa wanasema hawajaingia kwenye biashara kwa sababu hawana mitaji, hawana muda, hawana wazo zuri, hawana uzoefu au hawana mwongozo sahihi.

Lakini hizo zote siyo sababu za kweli, kwa sababu vitu vyote hivyo unaweza kuvipata kwa wengine hata kama wewe huna.

Kama huna mtaji unaweza kuupata kwa wengine kupitia njia mbalimbali kama michango, uwekezaji, ruzuku na hata mkopo.

Kama huna muda unaweza kutumia muda wa wengine kupitia kuwaajiri.

Kama huna wazo, mawazo ya biashara siku hizi ni kama chumvi, ni mengi na yapo kila mahali.

Kama huna uzoefu ni kitu ambacho unaweza kukipata kwa wengine, kwa kujifunza kwao au kutumia watu wenye uzoefu ambao wewe huna.

Na kama huna mwongozo sahihi, sijui nisemeje hapa, lakini maarifa yote sahihi kuhusu biashara yanapatikana kwa urahisi sana.

Kama unavyoona, sababu zote unazojipa zina majibu, ambayo unaweza kuyapata kama utayatafuta.

Lakini ipo sababu moja, ambayo umekuwa huitaji, lakini ukiikosa hiyo, huwezi kuipata kwa mtu mwingine yeyote yule. Hii lazima ianzie ndani yako, na kama haipo basi huwezi kuanza biashara na hata ukianza hutafika mbali.

Sababu hiyo moja ni mapenzi ya dhati kwenye kile kitu ambacho unakifanya.

Rafiki, kama huna mapenzi ya dhati kwenye biashara unayotaka kwenda kufanya, umeshashindwa kabla hata hujaanza.

Unapaswa kuipenda kweli, mapenzi ya dhati kutoka ndani ya moyo wako, yanayokupa msukumo mkubwa wa kupiga hatua hata pale unapokutana na magumu au changamoto mbalimbali.

Mapenzi ya dhati ni kitu ambacho huwezi kukipata kwa wengine kama hakijaanzia kwako. Hata kama utapata wafanyakazi wazuri kiasi gani, kama wewe mwenyewe huna mapenzi ya dhati kwenye biashara yako, wao pia hawataweza kuipenda na hivyo hawatasukumwa kujituma zaidi ya kawaida.

Na kama biashara unaipenda kweli, kama mapenzi ya biashara hiyo yanatoka ndani ya moyo wako, hutakubali kitu chochote kikuzuie kuianza. Kila kikwazo utakitafutia jawabu na utaweza kupiga hatua.

Hivyo basi rafiki, hebu jiambie ukweli, pale unaposema huwezi kuanza biashara kwa sababu huna muda, ni kweli huna muda au hupendi tu. Maana sielewi utasemaje huna muda huku unaumia mitandao ya kijamii, unafuatilia kila aina ya habari, unakula mara tatu kwa siku, unalala, na mengine kama hayo. Hayo yote unapata muda wa kuyafanya kwa sababu unayapenda. Hivyo penda biashara yako na muda au chochote kinachokukwamisha utakipatia jawabu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha