“I’ll never be ashamed to quote a bad writer with a good saying.”
—SENECA, ON TRANQUILITY OF MIND, 11.8
Ni siku mpya, siku nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Tumepata nafasi nyingine bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Asubuhi ya leo tutafakari JIFUNZE KWA KILA MTU NA KILA KITU…
Usibague unajifunza kwa watu gani au kwenye vitu gani,
Kuwa tayari kujifunza kwa mtu yeyote na kwa kitu chochote.
Hata kama mtu hukubaliani naye, kama kuna kitu cha kujifunza kwake basi usiache kujifunza.
Hekima ni hekima, haijalishi imetoka kwa nani.
Kama kuna kitu kizuri cha kujifunza, jifunze, usiangalie kimetoka kwa nani na kama unakubaliana naye au la.
Watu wengi wamekuwa wanakosa fursa nzuri za kujifunza kwa sababu tu hawakubaliani na watu wanaofundisha au kushauri.
Usiwe kwenye kundi hilo.
Ukweli haubadiliki kwa sababu umeletwa kwako na mtu usiyekubaliana naye.
Kuwa tayari kujifunza kutoka kwa kila mtu na kila kitu na kila wakati utajifunza mengi sana yatakayokuwezesha kuwa bora zaidi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujifunza kwa kila mtu na kila kitu, bila ya kubagua.
#NidhamuUadilifuKujituma #AfyaUtajiriHekima #KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1