Ukiona mtu aliyepiga hatua kuliko wewe anafanya kitu kwa kukirudia rudia, jua kina manufaa fulani kwake.
Hata kama hukubaliani na mtu huyo au kile anachofanya, jua kabisa kile anachofanya siyo kitu cha kijinga.
Kina manufaa fulani ndiyo maana anakifanya.
Na wewe unaweza kujifunza na ukakifanya pia, au ukakifanya kwa ubora zaidi.
Nakushirikisha hili rafiki kwa sababu watu ambao hawajafanikiwa ni mafundi wazuri wa kuwakosoa wale waliofanikiwa, kwa kuona wanachofanya siyo sahihi.
Lakini ukweli ni kwamba kama mtu amefanikiwa kuliko wewe, kuna kitu cha tofauti ambacho anakifanya, na huenda ni hicho unachokiona cha kijinga.
Unapoona mtu aliyefanikiwa sana anaendelea kuweka juhudi kubwa kwenye kazi zake, usijiambie huyo ni mjinga, ya nini ajisumbue wakati anaweza kupumzika tu. Jua hicho anachofanya ndiyo kimemfikisha hapo alipo, na hivyo anakiheshimu.
Unapoona biashara kubwa zinatumia fedha nyingi kurusha matangazo kwa njia mbalimbali, usiseme hawa wanapoteza tu fedha bure, jua matangazo hayo yanawalipa ndiyo maana wanayafanya. Kabla hujasema ni kitu cha kijinga, ni vyema ujifunze kupitia hilo ili na wewe uweze kufanya kwa ubora zaidi.
Ukiweza kuondokana na tabia ya kuona vitu wanavyofanya wengine ni vya kijinga na kuwa tayari kujifunza kupitia kila mtu na kile anachofanya, utaweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako.
Usijidanganye kwamba wewe ndiyo unajua sana kuliko wale ambao wanapiga hatua kupitia yale wanayofanya. Na kama unajua zaidi, basi unapaswa kuwa na matokeo zaidi ya hao wengine. Kama wao wana matokeo mazuri kuliko yako, weka ufahari wako pembeni na JIFUNZE.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,