Hakuna biashara mbaya, bali kuna wafanyabiashara wabaya.

Hakuna uwekezaji mbaya, bali kuna wawekezaji wabaya.

Hakuna mapenzi mabaya, bali kuna wapenzi wabaya.

Hakuna uongozi mbaya, bali kuna viongozi wabaya.

Tumezoea kulaumu hali kwamba ni mbaya, wakati hali hizo haziwezi kuwa na uzuri au ubaya, bali zinabeba kile ambacho kipo kwa mhusika wa hali hiyo.

Kila biashara ni nzuri, inategemea nani anafanya hivyo. Kadhalika kwenye vitu vingine kama uwekezaji, uongozi na mapenzi.

Ili kitu kiwe kizuri, lazima kwanza wewe mfanyaji uwe mzuri. Kama unataka biashara yako iwe nzuri na inayolipa, lazima kwanza wewe mfanyabiashara uwe mzuri, unayeielewa biashara yako na kuisimamia vizuri na hapo itafanya vizuri. Kama unafanya biashara kwa mazoea, huifuatilii kwa umakini, huisimamii vizuri, utakachopata ni matokeo mabaya, halafu utalaumu biashara ni mbaya, wakati wewe mwenyewe ndiye mbaya kwenye biashara hiyo.

Kitu chochote unachojihusisha nacho, kitakuwa kizuri au kibaya kulingana na jinsi ulivyo wewe mwenyewe. Kuwa mzuri na vitu vitakuwa vizuri, kuwa mbaya au mwenye udhaifu na vitu vitakuwa vibaya na dhaifu.

Kabla hujauliza ni biashara ipi nzuri kufanya, uwekezaji upi mzuri kufanya au kitu gani kizuri kwako kufanya, anza kujiuliza kwanza je wewe ni mtu mzuri kwa vitu hivyo? Uko tayari kufanya kwa utofauti, kujituma na kujisukuma sana kuliko wengine? Je upo tayari kujifunza na kukijua kitu hicho kwa kina?

Kama biashara ni mbaya, basi kuwa na uhakika wewe ndiye mbaya, badilika kwanza wewe na biashara yako itabadilika pia.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha