Mpendwa rafiki yangu,

Kina kutofautisha wewe na mbuzi ni kitu kimoja tu, kama macho mbuzi anayo kama wewe,masikio  anayo, mdomo anao hivyo kinachotutofautisha sisi na wanyama ni akili tu.

Sisi binadamu ni moja ya viumbe ambao tumependelewa sana na Mungu, kwa kupewa tu akili basi tunaweza kuwa bora kuliko wanyama wengine wote.

Kama sisi tumepewa uwezo mkubwa wa akili sasa kwanini tunashindwa malezi na hata na wanyama? Malezi ya watoto wengi siku hizi yamekuwa ni changamoto sana. Wazazi wanajua kuzaa tu lakini swala la kulea wanaona siyo jukumu lao.

Tunapaswa kujua kuwa malezi ni suala la baba na mama na siyo la yaya. Hatushiriki katika njia ipasayo ya kumlea mtoto, tunawaachia watu majukumu ya kulea watoto ambao wanakuwa wanaiga tabia ambazo hata wewe huna.

Watoto huwa wanajifunza tabia, kama uliyemwachia mtoto wako tabia zake ni mbaya jua kabisa baadaye ukiona mtoto anatabia ambazo siyo sawa, atakuwa amejifunza kwa hao uliowaachia.

Huwa ninapenda sana kuwachukulia mifano ya malezi kutoka kwa kuku na bata. Bata na kuku wote ni aina ya ndege lakini ndege hawa wana malezi ya tofauti kabisa na bata.

Tumuangalie bata katika malezi yake. Bata yeye malezi yake kwa watoto wake yanakuwa ni mabaya siyo ya kuigwa kabisa lakini kwa sasa binadamu wengi wanawalea watoto wao malezi ya bata.

Malezi ya bata yeye huwa anajijali yeye kuliko watoto wake, bata huwa yeye anakuwa mbele na kuwaacha watoto wake nyumba pasipo kujua usalama watoto wake. Akipata chakula anajiangalia yeye kwanza badala ya watoto wake.

Bata hajali watoto kabisa, hii tunaweza kujifunza hata kwa sisi binadamu je malezi unayompa mtoto wako ni ya bata au ya kuku?

Kuku yeye malezi yake ni mazuri sana, tunapaswa kuiga mifano mizuri kutoka kwa kuku. Kuku anawalea watoto wake kwa upendo. Anajitoa sadaka yeye huwa anakuwa nyuma na kuwatanguliza watoto mbele tofauti na bata. Akipata chakula anawapa watoto wake na siyo kujiangalia yeye kwanza.

Ni mara ngapi wazazi wanajiangalia wao tu, wengine wanakula vizuri nje wakija nyumbani watoto wanakula hovyo. Kile kizuri anachokula nje watoto wake hawali je huo ni upendo? Tunazidiwa hata na kuku?

SOMA; Hii Ndiyo Namna Bora Ya Kuendesha Familia Kwa Mafanikio Makubwa

Kuku huwa anawajali watoto wake, anawalinda dhidi ya maadui , anawakinga watoto wake na baridi na kujua kile kinachoendelea kwa watoto wake ukilinganisha na bata.

Tunapaswa kuwalea watoto wetu malezi mazuri kama ya kuku, tuache kuwalea watoto malezi ya bata. Malezi ya bata hayana nafasi katika karne hii ya ishirini na moja. Tuwe karibu na watoto wetu kama vile kuku anavyowajali vifaranga vyake.

Hatua ya kuchukua leo; kuwa na malezi bora ya mtoto. Jua mtoto ni malezi. Jitoa sadaka katika kumlea mtoto wako vizuri. Ukiweza kumlea mtoto wako vizuri katika dunia ya sasa utakua umempa zawadi nzuri sana.

Kwahiyo, walee watoto vema, wafundishe kweli ili kweli ije kuwasaidia baadaye. Usimfiche mtoto kwa karne hii, bali mwambie yale anayopaswa kujua kwani ukimficha dunia itamwambia na dunia inaweza ikamfundisha tofauti na wewe. Dunia huwa haijali, haina huruma hivyo tengeneza misingi imara kwa watoto wako.

Makala hii imeandikwa na

Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa  http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana