Leo hii ukapewa nafasi ya kuwa na mazungumzo ya dakika kumi na raisi wa nchi, zitakuwa ni dakika kumi ambazo utaziwekeza kwenye mazungumzo hayo. Hutatumia muda huo kuangalia simu yako, au kuangalia nini kinaendelea kwenye mitandao. Hata kama utaruhusiwa kuwa na simu, lakini hata ikiita, utaipuuza, hutataka hata kujua nani anapiga, kwa sababu upo kwenye mazungumzo ambayo ni muhimu sana.

Lakini unapokuwa unamhudumia mteja wa biashara au kazi yako kwa dakika hizo hizo kumi, utaruhusu usumbufu wa kila aina uingilie huduma yako. Simu ikiita utaacha kuongea na mteja na kuipokea, hata kama namba inayopiga huijui.

Kinachotofautisha mazungumzo haya ya aina mbili ni ule umuhimu ambao tunauweka kwenye mazungumzo hayo. Pale ambapo tunajua kwamba tunaongea na mtu muhimu, ambaye siyo rahisi kumpata kila wakati, tunalinda na kuheshimu sana muda wetu. Haturuhusu usumbufu wowote kuingilia. Lakini tunapoongea na mtu ambaye tunaona tunaweza kumpata muda wowote, tunaruhusu usumbufu.

Sasa leo nataka nikuulize swali moja, ni mtu gani muhimu sana kuliko wote duniani kwa upande wako? Najua hapa utakuja na mawazo mengi, wazazi, watoto, mwenza na kadhalika.

Lakini mimi nakwenda kukusaidia kubadili hilo. Tunajua jinsi gani fedha ilivyo muhimu kwenye maisha yetu, kwamba hata wale ambao tunasema ni wa muhimu, bila ya fedha mahusiano yetu na wao hayawezi kuwa bora.

Je, kuna mtu muhimu kwako zaidi ya yule ambaye anakupa fedha? Yule ambaye ananunua au kulipia kile unachouza au kufanya?

Huyu ndiye mtu muhimu kuliko wote kwenye dunia yako, kwa sababu ndiyo anakuwezesha wewe kula, kupeleka watoto shule, kulipa bili mbalimbali, kuvaa na kupata yale yote unayohitaji.

Hivyo basi, weka umuhimu na heshima kubwa kwa yeyote anayekuletea fedha. Iwe ni kwenye kazi au biashara, yule mteja ambaye ananunua unachouza au kufanya, ndiyo mtu wa muhimu zaidi kwako.

Unapopata nafasi ya kuongea naye au kumhudumia, chukulia kama upo na raisi wa nchi na hivyo umakini wako wote uweke kwa mtu huyo. Usiruhusu usumbufu wa aina yoyote uingilie hilo, sahau kila kitu na weka umakini wako wote kwa mtu huyo.

Utakapoanza kufanya hili, utashangaa jinsi ambavyo wateja watafurahia kuja kwako na kuhudumiwa na wewe, utashangaa wateja wanatamani kila wakati kurudi na watakuja na wengine pia.

Mbinu za kutoa huduma bora kwa wateja wako ni nyingi, lakini hii niliyokushirikisha leo, ya kumfanya mteja wako kuwa ndiyo mtu muhimu kuliko wote duniani pale unapokuwa naye, ni mbinu yenye nguvu kubwa sana. Itumie kila wakati.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha