Huwa tunaweka malengo na mipango yetu ya mafanikio kutoa A mpaka Z. Na tunataka mipango hiyo iende kama tunavyopanga, kuanzia mwanzo mpaka mwisho.
Lakini tunajua vyema ya kwamba hakuna mtu yeyote ambaye amewahi kuwa na njia ya mafanikio ya aina hiyo. Kila mtu anakutana na vikwazo na changamoto nyingi kabla hajapata kile hasa anachotaka.
Tunapokutana na vikwazo na changamoto mbalimbali kwenye safari yetu ya mafanikio, huwa tunachukia, tunakata tamaa na kuona hakuna tena namna ya sisi kufanikiwa.
Lakini hilo siyo sahihi, tunapokutana na vikwazo na changamoto, tunapaswa kufurahia na kukaribisha kwa mikono miwili.
Hii ni kwa sababu, vikwazo na changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha yako, vinakuja na manufaa kwako. Hakuna kikwazo unachopitia ambacho hakikufanyi kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa kabla ya changamoto hiyo.
Changamoto na magumu unayopitia yanakufanya ujue vizuri uwezo mkubwa uliopo ndani yako. Huwezi kujijua kama hujapitia majaribu makubwa.
Lakini pia vikwazo na changamoto hivi vinakukomaza kwa yale yanayokuja mbele yako. Pale unapofikia mafanikio makubwa, unakaribisha changamoto kubwa pia, hivyo vikwazo unavyopitia kabla ya kufikia mafanikio hayo makubwa, zinakuandaa kukabiliana na changamoto zinazokuja na mafanikio makubwa.
Pia wapende sana wale wanaokuchukia, wanaokupinga, wanaokubeza, wanaokukwamisha na hata wanaokuangusha. Ni rahisi kuwalaumu na kuona bila ya wao ungekuwa umepiga hatua sana. Lakini ukweli ni kwamba, kupitia wao utaweza kupiga hatua kubwa sana.
Maana hao ndiyo watakusukuma wewe kufanya zaidi, ili uwaoneshe inawezekana, ili wajue kwamba unaweza na ili ukatae utabiri wao juu yako. Kama kila mtu anakubaliana na wewe kwa kila unachofanya ni vigumu sana kupata msukumo wa kufanya kitu cha tofauti, utaishia kufanya kile ambacho umezoea kufanya.
Kila unapokutana na ugumu au changamoto kwenye maisha yako, furahi na karibisha hali hiyo, na swali kubwa kwako linapaswa kuwa hili, ni manufaa gani ninayokwenda kuyapata kupitia changamoto hii? Na hapo utaona jinsi unavyoweza kujifunza na kunufaika.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,