Uhuru na utumwa unaendana na werevu na upumbavu.

Ukiwa mwerevu ni rahisi sana kuwa huru, ukiwa mpumbavu lazima uwe mtumwa.

Tofauti ya mwerevu na mpumbavu inayozalisha uhuru au utumwa ni hii;

Mwerevu hakuna chochote anachokitaka, bali anafurahia kila anachokipata na kukitumia vizuri. Hakuna kitu chochote ambacho mwerevu anaweza kusema hawezi kuishi bila ya kuwa nacho. Anajua vitu vinakuja na kupita hivyo anavitumia wakati vipo na vinapoondoka anajua wakati wake umefika hivyo hang’ang’ani viendelee kuwepo.

Mpumbavu anataka kila kitu na anataka awe nacho kwa namna anavyotaka yeye. Mpumbavu hakubali pale anapokosa kitu, anajiumiza na kuhangaika kupata kila anachotaka, hata kama kimepitwa na muda wake. Kwa kifupi mpumbavu hakubaliani na matokeo, anataka kila kitu kiende kama anavyotaka yeye, dunia iende kama anavyotaka yeye.

Kwa tofauti hizi mbili, mwerevu anakuwa huru mara zote, kwa sababu haweki mategemeo yake kwenye kitu chochote ila yeye mwenyewe. Huwezi kumtishia mwerevu kwa chochote, kwa sababu hakuna chochote anachokitaka au kukitegemea sana.

Lakini kwa upande wa mpumbavu, ni rahisi kumfanya kuwa mtumwa, unachopaswa kufanya ni kushikilia kile anachokitaka sana, kile anachojiambia hawezi kuishi bila ya kuwa nacho. Halafu sasa unakuwa unampa kitu hicho kwa masharti yako mwenyewe. Hapa mpumbavu atakuwa mtumwa wako, atafanya kila unachomwambia afanye ili tu apate kile anachotaka sana.

Epuka kuwa mpumbavu kama unataka kuwa huru. Na hatua ya kwanza ni kuondoa matakwa na mategemeo yako kwenye kitu chochote cha nje.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha