“Success comes to the lowly and to the poorly talented, but the special characteristic of a great person is to triumph over the disasters and panics of human life.”
—SENECA, ON PROVIDENCE, 4.1

Hongera sana mwanamafanikio kwa nafasi hii nzuri sana tuliyoipata leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee wana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KILA MTU ANAWEZA KUPATA BAHATI, SIYO KILA MTU ANAWEZA KUVUMILIA…
Tunawajua watu kwenye maisha ambao kila mara wanakutana na bahati.
Watu ambao shuleni walikuwa hawasomi sana, lakini kwa namna fulani wakafaulu.
Watu ambao kazini hawajitumi sana, lakini kwa namna fulani wanapandishwa vyeo na kupewa nafasi za juu zaidi.
Watu ambao hawana malengo wala mipango mikubwa ya maisha, wanajiendea tu, lakini wanakutana na fursa kubwa na zinazowanufaisha sana.

Tunapowaona watu wa aina hii, ni rahisi kujiambia kwamba mafanikio hni bahati, kama huna bahati huwezi kufanikiwa.
Ni rahisi kukubaliana na wale wanaosema maisha hayana fomula, kwa sababu unawaona ambao hawajajioanga wanafanikiwa.
Ni rahisi kukubali kwamba kama ipo ipo tu, kwamba kama umepangiwa basi utapata na kama hujapangiwa hupati, hata ufanye nini.

Lakini fikra zote hizo siyo sahihi, wachache kukutana ma bahati haifanyi bahati kuwa kanuni kuu ya maisha.
Lakini pia kumbuka ni watu gani tunaowaangalia na kuwaona mashujaa kwenye maisha?
Je ni wale ambao maisha yao yameenda kwa bahati au wale ambao wamekutana na magumu, wakapambana, wakang’ang’ana na mwisho kushinda?

Majibu yako wazi, tunawaangalia wale ambao wameweza kupambana licha ya kukabiliana na magumu.
Tunawaangalia wale ambao wameanzia chini kabisa, wakakutana na magumu, wakapambana na kufanikiwa.
Wakati wengine wanakata tamaa, wachache hao waling’ang’ana mpaka kufanikiwa.
Watu wa aina hii ni wachache wana, lakini pia ndiyo wanaoleta matumaini kwa wengine kwamba inawezekana.

Kuwa mmoja wa watu hawa, kuwa king’ang’anizi, pambana mpaka upate kile unachotaka.
Kumbuka azimio ni kupata unachotaka au kufa ukiwa kwenye mapambano ya kukipata. Hakuna kukata tamaa, hakuna kurudi nyuma. Mambo mazuri yako mbele yako.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kupambana na kung’ang’ana moaka kupata unachotaka na siyo kutegemea bahati.
#WekaMapambano #BahatiSiyoKanuni #Ung’ang’aniziUnalipa

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1