Huwa tunasema maisha ni kama biashara, kwamba ukiyaendesha maisha yako kwa misingi ambayo unaendesha nayo biashara yako, basi yatakuwa na mafanikio makubwa.

Pia tunasema biashara nayo ni maisha, kwamba biashara ni kitu kinachozaliwa, kinakua na pia kinakufa. Biashara huwa ina maisha yake, ambayo yakizingatiwa inadumu na yakipuuzwa inakufa.

Lakini kuna tofauti moja kubwa kati ya maisha na biashara, ambayo tunapaswa kuijua na kuitumia vizuri. Tofauti hiyo ni kwenye huruma na usawa.

Maisha yana huruma, lakini hayana usawa. Unaweza kufanya kila kitu kwa usahihi na bado ukakutana na kitu ambacho hukutegemea kukutana nacho. Mfano unaweza kujitunza vizuri na kuishi kwa misingi ya afya, lakini ukaishia kupata saratani ya mapafu au uvimbe kwenye ubongo. Wakati kuna mtu mwingine ambaye anaishi bila kujali, ni mlevi, mvutaji wa sigara na tabia nyingine hatarishi, lakini asipate magonjwa hayo. Pamoja na kukosekana kwa usawa huu, lakini maisha yana huruma, watu wataumia na wewe, watalia na wewe na kukufariji.

Biashara ina usawa, lakini haina huruma. Kama biashara itaendeshwa kwa misingi ambayo ni sahihi, ikawa na wateja wenye uhitaji, ikafanya mauzo, gharama za mauzo na za kuendesha biashara zikawa chini, basi biashara hiyo itatengeneza faida. Haijalishi biashara hiyo ni kubwa au ndogo, nzuri au mbaya, misingi inapofuatwa matokeo mazuri yanazalishwa. Hivyo biashara ina usawa mkubwa sana. Lakini haina huruma, unapofanya makosa hakuna kupewa nafasi ya pili, biashara inakupoteza kabisa. Na biashara yako inapokufa leo, hakuna hata anayejali, biashara ni nyingi zinazoanzishwa na kufa. Pia biashara haina huruma kwenye muda wako ambao inahitaji, biashara inaweza kusimamisha kabisa maisha yako mengine, inataka muda wako wote, usahau vitu vingine vyote na kuweka umakini wako kwenye biashara hiyo.

Kwa kujua tofauti hii kubwa kati ya maisha na biashara, kunapaswa kukusaidia kujua hatua sahihi za kuchukua kwenye maeneo hayo mawili. Kwenye maisha kuna mambo yatatokea nje kabisa ya uwezo wako, yapokee na kwenda nayo, usiyalalamikie. Kwenye biashara kuna wakati utahitajika kufanya kazi kama mtumwa, pokea hilo kwa mafanikio ya biashara yako.

Huruma na usawa ni vitu unavyopaswa kujua wakati wa kuvitumia na wakati unapovikosa ili maisha yako yawe na utulivu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha