Kitu kimoja ambacho sisi binadamu huwa hatukipendi ni mabadiliko. Huwa tunapenda kufanya kile ambacho tumezoea kufanya kwa sababu tuna uhakika wa matokeo tunayokwenda kupata. Hatupendi kubadilika na kufanya vitu vipya kwa sababu hatuna uhakika wa matokeo tunayokwenda kupata.

Lakini mabadiliko ndiyo kitu pekee ambacho hakibadiliki kwenye maisha yetu. Yaani kila kitu kwenye maisha yetu kinabadilika, isipokuwa mabadiliko. Mabadiliko ni lazima, iwe unataka au hutaki.

Kuliona hili vizuri, jaribu kuyaangalia maisha yako tangu unazaliwa mpaka hapo ulipofika sasa. Kuzaliwa kwako kwenyewe kulikuwa ni mabadiliko makubwa, uliyaacha maisha ya kukaa tumboni mwa mama yako na kuingia maisha ya duniani. Hukupenda mabadiliko hayo ndiyo maana kitu cha kwanza ulichofanya baada ya kuzaliwa ni kulia.

Ulipozaliwa hukuwa unaweza kufanya chochote, kazi yako ilikuwa ni kunyonya, kulia na kulala. Lakini kadiri siku zilivyokwenda ndivyo mabadiliko yalilazimishwa kwako. Ulifika wakati ikabidi ukae, japo hukupenda, kusimama, kutembea na mengine. Yote hayo mwanzoni hukuyapenda, uliumia, ulianguka lakini hukurudi nyuma.

badilika kabla hujabadilishwa..jpg

Cha kushangaza sasa, sisi binadamu tunapofikia utu uzima, tunayaogopa zaidi mabadiliko kuliko tulivyokuwa watoto. Inakuwa vigumu sana kwetu kubadilika kwa hiari yetu wenyewe na kujiambia labda mambo yatakwenda vizuri.

Unakuta mtu yupo kwenye kazi au biashara kwa zaidi ya miaka kumi, kazi hiyo haipendi, haifanyi kwa moyo na haimlipi vizuri, lakini hakuna hatua za tofauti anazochukua. Kwa sababu anakuwa anategemea huenda siku moja mambo yatakuwa vizuri, lakini mambo yanaendelea vile vile.

Unakuta mtu yupo kwenye mahusiano ambayo yanampa changamoto kila siku, hakuna kuelewana, hakuna amani, lakini hakuna hatua anazochukua kuleta mabadiliko katika hali hiyo.

Kwa upande wa fedha, unakuta mtu ana kipato kidogo, ana matumizi makubwa ambayo yanazidi kipato chake na kama hiyo haitoshi, ana madeni ambayo yanaendelea kukua. Hakuna mabadiliko yoyote makubwa mtu huyu anayafanya zaidi ya kuendesha maisha yake kwa mazoea, kitu ambacho hakimwongezei kipato, lakini kinaongeza madeni yake.

Kwa kuwa maisha hayaendi kama unavyotaka, mabadiliko huwa yanatokea, iwe unataka au hutaki.

SOMA; Mtu Huyu Mmoja Ndiye Anayekukwamisha Wewe Usifanikiwe Zaidi, Na Hapa Kuna Mbinu Za Kumvuka Asikukwamishe Tena.

Kuna nyakati tatu za kufanya mabadiliko kwenye maisha yako.

Wakati wa kwanza ni pale maumivu ya ndani yanapokuwa makubwa na hayavumiliki tena. Hapa maumivu unayopata kwa kutokubadilika yanakuwa makubwa sana kiasi kwamba hayavumiliki tena. Hapa unakuwa huna budi bali kubadilika, kwa sababu kwa kutokubadilika unaumia na kupotea zaidi. Wengi hulazimishwa kubadilika pale maumivu wanayopata ni makubwa, lakini kama wewe utasubiri mpaka maumivu yakuzidi ndiyo ubadilike, utakuwa umejichelewesha sana. Yaani ni kama kuchagua kuyapata maumivu wakati kuna njia mbadala.

Wakati wa pili ni pale mazingira ya nje yanapokuwa yamebadilika sana kiasi kwamba huwezi kuendana nayo kama na wewe hujabadilika. Hapa unalazimishwa kubadilika kutokana na mazingira ya nje. Kila ambacho umekuwa unategemea kinakuwa hakifanyi kazi tena kama ulivyokuwa unategemea na hivyo inakubidi tu ubadilike. Kama utalazimishwa kubadilika na nguvu za nje, jua umeshachelewa sana na huenda mabadiliko utakayofanya yasilete tija kwako.

Wakati wa tatu wa kubadilika ni pale unapoamua wewe mwenyewe na kusema IMETOSHA SASA. Hapa unachukua maamuzi ya kubadilika mara moja na kuyasimamia. Kama ni kitu ulikuwa unafanya unajiambia hukifanyi tena na kweli hukifanyi tena. Kama kuna kitu unachopaswa kufanya lakini hukifanyi unajiambia unaanza kukifanya na unafanya kweli. Aina hii ya mabadiliko inahitaji kujitoa kweli, na inahitaji nidhamu ya hali ya juu, kwani mabadiliko ya aina hii huwa hayana kubembeleza. Haya ni mabadiliko yanayokuwezesha kuendana na hali kabla mambo hayajakuacha sana.

Ninachokusihi wewe rafiki yangu ni kutumia njia ya tatu kubadilika, kama kuna chochote ambacho hakikupi matokeo unayotegemea kupata, ni wakati wa wewe kubadilika sasa. Jiambie IMETOSHA SASA na anza kufanya vitu kwa utofauti. Haitakuwa rahisi, utakutana na vikwazo vingi, lakini unapofanya maamuzi na kuyasimamia, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata matokeo bora.

SOMA; Kweli Tatu Chungu Unazopaswa Kuzijua Kuhusu Dunia Ili Uwe Na Maisha Ya Utulivu Na Mafanikio.

Swali muhimu kwako rafiki yangu, je ni maeneo gani kwenye maisha yako unayopaswa kujiambia IMETOSHA SASA na kuanza kuchukua hatua za tofauti kwenye maisha yako? Jiulize na upate majibu sahihi ya swali hilo na kisha chukua hatua sahihi leo hii, siyo kesho, ni leo, ni sasa.

Na kwa kuwa mimi rafiki yako nimekuwa nashirikiana na watu kama wewe kwa muda mrefu sasa, najua eneo moja unalohitaji kujiambia IMETOSHA SASA, na kuchukua hatua za tofauti. Eneo hilo ni fedha. Tabia zako za kifedha ulizonazo sasa ndiyo zinakukwamisha usipige hatua. Kama unataka kutoka hapo ulipo sasa, lazima ujiambie IMETOSHA SASA, na uchukue hatua za tofauti kwenye hali yako ya kifedha. Mfano kudhibiti matumizi yako, kuanza kujilipa wewe mwenyewe kwanza, kuongeza kipato chako, kuacha kukopa, kuanzisha biashara, kuwekeza na mengine muhimu.

Kama leo umejiambia IMETOSHA SASA kwa upande wa fedha, basi chukua kitabu chako cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA na ukisome. Kama umeshakipata najua hujapata muda mzuri wa kukisoma kwa usongo wa kutaka mabadiliko ya kweli, hebu tumia siku ya leo kufanya hivyo.

Na kama bado hujapata kitabu hiki muhimu sana kwenye mabadiliko yako ya kifedha, piga simu 0678 977 007 na utatumiwa au kuletewa nakala yako ya kitabu popote pale ulipo Tanzania.

Imetosha sasa, shika hatamu ya maisha yako kwa kubadili chochote ambacho hakiendi kama unavyotaka wewe. Anza na fedha zako, anza na kitabu ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, piga 0678 977 007 kukipata.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

elimu fedha 2