Kuna viungo vitatu vinavyochochea hofu kwenye maisha yako.
Ukivijua viungo hivi na kuchukua hatua sahihi kwa kila kiungo, hutasumbuliwa tena na hofu. Utaweza kufanya maamuzi sahihi huku ukiwa na utulivu wa ndani.
Wale wanaojua kutumia vizuri viungo hivi vitatu, huweza kuwapa wengine hofu na hivyo kuwasukuma kufanya maamuzi ambayo yana manufaa kwao na siyo kwa wale wanaofanya maamuzi hayo.
Kiungo cha kwanza ni muda, muda ni chanzo kikubwa cha hofu, hasa pale unapoona ya kwamba huna muda wa kutosha kufanya kile unachotaka kufanya, au kupata unachotaka. Tunaishi zama ambazo muda ni mdogo na mambo ya kufanya ni mengi, hivyo kama utakuwa unauhesabu muda kwa namba hiyo, kila wakati utakuwa kwenye hofu. Kila unapokazana kufanya mambo mengi kwenye muda mchache ulionao, ndivyo unavyozidi kuwa na hofu kwamba kuna mengine hutaweza kuyafanya. Halafu kuna upande wa pili wa hili ambapo ni wengine kukushinikiza kufanya maamuzi ndani ya muda mfupi, wakikuambia kwamba ukisubiri utakosa fursa nzuri. Kukabiliana na kiungo hiki, kwanza weka vipaumbele vyako vizuri, fanya yale ambayo ni muhimu pekee na mengine achana nayo. Na mara zote jua una muda wa kutosha, kama kuna kitu watu anakuambia uchukue hatua haraka usikikose, achana nacho. Kamwe usifanye maamuzi yoyote kwa kusukumwa na muda.
Kiungo cha pili ni kujishikiza, chochote unachojishikiza nacho, kinakupa hofu. Pale unapojiambia siwezi kuishi bila ya kitu fulani au mtu fulani, hapo unakuwa umejiweka kwenyewe kwenye hofu. Hatari yoyote ya kupoteza kile ambacho umejishikiza nacho, inakupa hofu kubwa ndani yako. Na pale unapokipoteza kweli, inaleta mvurugo mkubwa katika utulivu wako. Na hata wale wanaotaka kukudhibiti, wakishajua kile ulichojishikiza nacho, kazi yao inakuwa rahisi, wanakutishia tu kwamba utakipoteza, na hapo inabidi ufanye kile wanachotaka ufanye, ili usipoteze ulichojishikiza nacho. Kukabiliana na hili, usijishikize na kitu chochote, yafanye maisha yako kuwa huru kwa kuwa tayari kupoteza chochote ambacho unakitumia na kukitegemea sana kwa sasa.
Kiungo cha tatu ni matarajio, kadiri unavyokuwa na matarajio makubwa, ndivyo unavyojiweka kwenye hofu kama hutayafikia. Unapokuwa na matarajio fulani na unataka yatokee kama ulivyopanga, unajiweka kwenye hali ya kukosa utulivu, mara zote kuwa na hofu kama yasipotokea. Na hata wale wanaotaka kukudhibiti, wakishajua unatarajia nini, basi wanatumia matarajio hayo kukulazimisha kuchukua hatua zenye manufaa kwao. Kukabiliana na hili, kuwa na matarajio, lakini usijiwekee uhakika wa asilimia 100 na hata kutegemea kila kitu kiende kama unavyotarajia. Weka nafasi ya mambo kwenda tofauti na ulivyopanga na kutarajia, na pale hayo yanapotokea hayatakuyumbisha.
Kama unataka kuikabili hofu, fanyia kazi viungo hivi vitatu na utaweza kuwa na utulivu mkubwa sana bila ya kujali nini kinachoendelea kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,