Pale mambo yako yanapokuwa magumu,

Pale unapokutana na changamoto kubwa na kuona kama huwezi kuvizuka.

Pale malengo na mipango yako inashindikana na matokeo unayoyapata siyo uliyotarajia,

Ndiyo wakati sahihi kwako kurejea kwenye chakula bora cha akili ambacho pia ni dawa ya roho yako.

Chakula hicho ni vitabu, vitabu bora ambavyo vimekuwepo kwa muda mrefu na kuendelea kusimama kutokana na ukweli ambao vitabu hivyo vimebeba.

Vitabu vya dini yoyote unayoamini vinaingia kwenye kundi hili, vitabu vya falsafa mbalimbali za kale vinaingia hapo pia. Na hata vitabu vingine vyenye mafunzo mbalimbali kuhusu fedha, biashara, mafanikio na hata taaluma fulani, na vimekuwepo kwa muda mrefu na watu bado wanavitumia kwa rejea, basi ni vitabu sahihi kwako.

Vitabu ni chakula sahihi cha akili, vinaipa akili kitu cha kufikiri na kuifanya kukua zaidi. Kupitia kujifunza unakuwa imara na kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Vitabu pia ni dawa ya roho, vinaponya majeraha yoyote ambayo roho yako imeyapata kupitia kushindwa, kukatishwa tamaa na hata kuchoka wewe mwenyewe.

Kila unapokuwa, kuwa na kitabu, kila siku soma kurasa chache za kitabu.

Usikubali kuishindisha na kuilaza akili yako na njaa, pia usikubali roho yako ibaki na maumivu, pata chakula bora kwa akili na dawa ya roho kwa kusoma vitabu.

Upande wa pili, tuna vyakula vibaya kwa akili na sumu kwa roho, ambavyo ni habari mbalimbali. Ukiwa mfuatiliaji mkubwa wa habari, hakuna kikubwa unachojifunza, lakini kila wakati utakuwa kwenye hali ya hofu. Kwa sababu habari nyingi ni hasi na za hofu. Epuka sana habari kama hutaki kuchosha akili yako na kuumiza roho yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha