Ushauri wa zamani kwenye mafanikio ulikuwa ni uyajue madhaifu yako, kisha ukazane kuwa imara kwenye madhaifu hayo.

Lakini kitu kimoja kilitokea kwa wale waliofuata ushauri huo, madhaifu yao yalizidi kuwa imara, na yale ambayo walikuwa imara wakawa dhaifu. Hivyo wakaishia kuwa vibaya kuliko walivyokuwa awali.

Ushauri wa sasa kwenye mafanikio ni kujua maeneo ambayo una uimara na kukazana kuwa imara zaidi maeneo hayo, na yale maeneo ambayo una udhaifu kutokujisumbua nayo.

Kwa kufuata ushauri huu, unakuwa imara sana kwenye maeneo machache, na mengine unakuwa dhaifu. Lakini uimara wako kwenye maeneo hayo machache, unafunika ule udhaifu ulionao kwenye maeneo mengine.

Na hapa ndipo udhaifu wako unapokuwa na manufaa kwako, unapochangia kwenye uimara wako, kwa kuutambua na kutohangaika na udhaifu ulionao.

Turudi kwenye mifano ili kuelewa hili vizuri.

Mainjinia wanao uwezo wa kutengeneza gari ambalo ni imara na lenye viwango sana kiasi kwamba hata lipate ajali ya aina gani, waliopo ndani ya gari hilo hawawezi kuumia kabisa.

Lakini sasa, kwa uimara huo wa gari, litakuwa zito sana kiasi kwamba halitaweza kuwa na mwendo wowote na pia litakuwa pana sana kiasi kwamba haliwezi kuenea barabarani.

Kwa hiyo tuko tayari kuyaweka maisha yetu hatarini, ili tuweze kupata mwendo wa kutoka eneo moja na kwenda eneo jingine.

Hivi pia ndivyo unavyopaswa kuyachukulia maisha yako, kuna baadhi ya manufaa unapaswa kuwa tayari kuyaacha yaende kwenye madhaifu uliyonayo na kupeleka nguvu zako kwenye uimara ulionao.

Ukishaujua udhaifu wako na kutokuuruhusu ukusumbue unageuka kuwa uimara kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha