Kwenye hesabu, msingi mkuu kabisa ambao kila mtu anapaswa kuujua ni MAGAZIJUTO. Magazijuto ni kifupi cha MAbano, GAwanya, ZIdisha, JUmlisha na TOa. Ukijua msingi huu unaziweza hesabu zote muhimu na kuweza kuyaendesha maisha yako vizuri.

Kwa msingi huo huo wa hesabu, tunaweza kupata msingi muhimu wa kuyaendesha maisha yetu, ambao utatupa utulivu mkubwa sana. Msingi huo ni kama ifuatavyo;

MABANO; Maisha yako yana mambo yaliyo ndani ya uwezo wako na yaliyo nje ya uwezo wako. Wewe pambana na yale mambo ambayo yako ndani ya uwezo wako, yaliyo nje ya uwezo wako achana nayo, yasikusumbue kabisa. Haya ndiyo mabano ya maisha yako, hangaika na ya ndani, achana na ya nje.

GAWANYA; Pale unapokabiliana na kitu chochote kikubwa na kinachokupa hofu ya kukianza, gawanya. Gawa jukumu kubwa kwenye vipande vidogo vidogo na anza kuchukua hatua kwenye kila kipande. Kama una lengo kubwa ligawe kwenye mipango midogo midogo na chukua hatua. Chochote kinachokupa hofu sasa, hebu kigawanye na hofu hiyo itapotea kabisa.

ZIDISHA; Kila unachopanga kwenye maisha, ili kuwa upande salama, zidisha zaidi ya unavyotegemea. Unapojiwekea malengo, zidisha mara kumi zaidi, na hii itakusukuma zaidi katika kuyafanyia kazi malengo hayo. Unapopanga bajeti ya kukamilisha kitu, zidisha mara mbili zaidi, mara zote bajeti huwa hazitoshelezi. Na unapotenga muda wa kukamilisha kitu, zidisha mara tatu zaidi, maana vitu huwa vinachukua muda mwingi kuliko tunavyopanga.

JUMLISHA; Ili maisha yako yawe bora, unapaswa kujumlisha watu na vitu vinavyoyafanya maisha kuwa mazuri. Kuna vitu ukivifanya unajisikia vizuri, kuna watu ukiwa nao unajisikia vizuri, hao ndiyo watu na vitu vya kujumlisha kwenye maisha yako.

TOA; Uhuru kwenye maisha unatokana na kutoa, kadiri unavyotegemea vitu vichache kwenye maisha yako, ndivyo unavyokuwa huru. Kadiri unavyoondoa mahitaji yasiyo na msingi, ndivyo unapata muda, nguvu na fedha nyingi kufanya yale muhimu kwako. Na kadiri unavyoondoa yale yasiyo muhimu, ndivyo unavyopata muda zaidi kwa yale muhimu.

Hayo ndiyo MAGAZIJUTO ya maisha yako, sasa kazi ni kwako, na leo chukua hatua hizo, jua mabano yako ni yapi, gawanya kila kinachokupa hofu, zidisha mipango yako, jumlisha mazuri na toa yasiyo mazuri.

Swali la kujiuliza na kujipa jibu leo, je ni kitu gani kimoja ambacho ukikitoa kwenye maisha yako yatakuwa bora sana?

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha