Huwezi kujenga nyumba bila ya kuwa na ramani, kwa sababu hutajua ni kitu gani unachokwenda kujenga.

Lakini inashangaza namna watu wengi wanavyoingia kwenye biashara huku wakiwa hawana ramani ya kuwawezesha kufanikiwa kwenye biashara hizo.

Ramani ya kufanikiwa kwenye biashara ni mchanganuo wa biashara hiyo, huo ndiyo unakuonesha biashara iko wapi, inakwenda wapi na itawezaje kufika kule inakokwenda.

business models.jpg

Bila ya mchanganuo wa biashara, huwezi kufanikiwa kwenye biashara hiyo.

Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara kwa mazoea. Wanapata wazo la biashara baada ya kuona wengine wanafanya biashara hiyo na kujiambia itakuwa inalipa. Wanaingia kwenye biashara hiyo wakiwa hawana mpango wowote wa ukuaji wanaoufanyia kazi.

Na haishangazi kwa nini biashara nyingi zinashindwa kufanikiwa, kwa sababu hazina ramani ya mafanikio.

Seth Godin ambaye anajulikana kama baba wa masoko, amekuwa akihubiri njia bora ya kufanya masoko kwenye biashara, njia ambayo siyo ya kupiga kelele, kutishia au kutamanisha. Bali ni njia ya kujua hitaji la wateja, kuwapa hitaji hilo kwa namba bora kabisa ambayo hawawezi kuipata kwa wengine, na wao wawe mabalozi wazuri wa biashara yake.

Kwenye kitabu chake kinachoitwa THIS IS MARKETING, Seth Godin ametushirikisha kila tunachopaswa kujua kuhusu ufanyaji wa masoko wa kistaarabu, ambao unajenga biashara yenye heshima na inayoaminika ka wengi.

Kwenye moja ya sura za kitabu hicho, Seth ametushirikisha mchanganuo bora wa biashara ambao unaiwezesha biashara yoyote ile kufanikiwa sana. mchanganuo huo una vipengele vitano, ambavyo vikifanyiwa kazi biashara inakuwa bora sana na inayofanikiwa zaidi.

Karibu tujifunze vipengele vitano vya mchanganuo bora wa biashara yenye mafanikio.

KIPENGELE CHA KWANZA NI UKWELI.

Kipengele cha kwanza kinaeleza ukweli kama ulivyo bila ya kuficha chochote. Kwenye kipengele hiki unaeleza hali ya mambo, jinsi ambavyo dunia inakwenda kwenye biashara unayofanya. Kipengele hiki kinaeleza uhalisia wa soko, hitaji ambalo lipo, washindani waliopo kwenye soko hilo, teknolojia zinazopatikana na pia jinsi ambavyo wengine wamefanikiwa au kushindwa kwenye soko hilo.

Kwenye kipengele hiki hupaswi kufanya makadirio wala makisio yoyote, bali unapaswa kueleza ukweli jinsi ulivyo. Na kadiri unavyokuwa makini, ndivyo inavyosaidia kuuona ukweli. Kadiri unavyojua vitu kwa undani zaidi, ndivyo unavyouona ukweli na kuielewa vizuri biashara hiyo.

Lengo kuu la kipengele hiki ni kuhakikisha kwamba unaielewa dunia inavyokwenda kwenye biashara husika, na hivyo kuweza kufanya maamuzi sahihi.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu; Street Smarts (Nyenzo Zote Muhimu Kwa Wajasiriamali Wanaotaka Kufanikiwa).

KIPENGELE CHA PILI NI AHADI.

Kwenye kipengele cha ahadi unapata nafasi ya kueleza ni jinsi gani unakwenda kubadili hali ilivyo. Baada ya kuujua ukweli, na kuona udhaifu uko wapi kwenye soko, hapo sasa unaweza kuahidi ni kipi unachokwenda kufanya tofauti. Hapa unatoa ahadi kwa wateja wako kwamba watakapofanya jambo X basi jambo Y litatokea.

Kwenye kipengele hiki unatengeneza msongo kwa wateja wako kupitia hadithi unazotengeneza. Unatengeneza mategemeo makubwa kwa wateja kwa kuja kwako. Unawapa nafasi ya kuamini kwamba mambo yanaweza kuwa bora zaidi ya yalivyo sasa.

Kipengele cha AHADI ndiyo moyo wa mchanganuo wa biashara, kwa sababu hapa ndipo penye sababu kuu kwa nini umeanzisha biashara husika, hapa ndipo penye kile kinachokutofautisha wewe na wafanyabiashara wengine, kinachowafanya wateja waje kwako na wasiende kwa wengine wanafanya biashara kama yako.

Unachopaswa kujua ni kwamba siyo kila utakachoahidi kitatokea kama ulivyoahidi, kuna mambo mengi yatakayokwenda tofauti na ulivyokuwa umepanga. Hivyo kuhakikisha huwaangushi wateja kwa ahadi zako, kipengele cha nne kinahusika.

KIPENGELE CHA TATU NI MBADALA.

Kwenye kipengele cha mbadala unatoa nafasi ya kufanya marekebisho pale ambapo ahadi yako haijatimia. Hapa unaonesha ni uhuru au utayari wa kubadilika kiasi gani ambao bidhaa, huduma au timu yako inayo.

Kwenye kipengele hiki cha mbadala, ndipo unaondoa ule wasiwasi ambao wateja wanao, kwa sababu wameshaahidiwa vitu vingi sana huko nyuma, lakini wamekuwa hawavipati.

Wewe unapokuwa na mbadala kwa mteja, na kuweza kumhakikishia kwamba haijalishi nini kimetokea lazima apate kile anachotarajia kupata, imani ya wateja juu yako na biashara yako inakuwa kubwa sana.

Kwenye kila ahadi unayotoa kwa wateja wako, hakikisha unawaonesha njia mbadala, kama ulichopanga kitashindwa, ni kwa namna gani wao hawatakwama.

KIPENGELE CHA NNE NI WATU.

Kipengele cha watu kina pande mbili;

Upande wa kwanza ni timu yako, hapa unaeleza wale watu ambao wapo au watakuwepo kwenye biashara yako. Unaelezea sifa wanazokuwa nazo ili kuweza kutengeneza timu bora na yenye ufanisi mkubwa kwenye biashara hiyo. Upande huu pia unaonesha mtazamo, tabia na hata sifa wanazokuwa nazo watu hao. Timu yako ndiyo inayochangia sana kwenye mafanikio ya biashara.

Upande wa pili ni wa wale unaowahudumia, wateja wa biashara hiyo. Hapa unaeleza kwa kina wale watu ambao biashara yako inawalenga, uhitaji walionao na jinsi ambavyo biashara yako inatimiza uhitaji wao. Kipengele hiki kinaeleza sifa za wateja hao, siyo tu za nje, kama eneo wanalopatikana na uwezo wao, bali pia sifa za ndani kama namna wanavyofikiri na mtazamo walionao.

Kadiri unavyoweza kuwaelezea wateja wako vizuri, ndivyo unavyoweza kuwafikia na kuwahudumia vizuri. Kumbuka hakuna biashara ambayo mteja wake ni mtu yeyote, kila biashara inapaswa kuwa na aina fulani ya wateja inayowalenga, hawa unawaelezea kwenye kipengele hiki cha watu.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE SMALL BUSINESS BIBLE (Kila Kitu Unachopaswa Kujua Ili Kufanikiwa Kwenye Biashara Ndogo).

KIPENGELE CHA TANO NI FEDHA.

Kipengele cha mwisho na ambacho wengi hupenda kukitolea macho zaidi ni fedha. Kwenye kipengele hiki unaeleza ni kiasi gani cha fedha kinachohitajika kuanzisha na kuendesha biashara hiyo. Pia kitaeleza ni jinsi gani fedha hiyo itakavyotumika kwenye biashara hiyo. Kipengele hiki huwa kinakuwa na makisio na makadirio mengi kwenye mzunguko wa fedha, taarifa za mapato yanayotarajiwa kutengenezwa na hata hesabu za mizania. Kipengele hiki kinahusika pia na kuweka makisio ya faida itakayopatikana na hatima ya biashara hiyo, kama itauzwa kwa biashara kubwa, itageuzwa kuwa ya umma au itabaki kuwa binafsi.

Kipengele cha fedha ndiyo kinaonesha jinsi ambavyo ramani uliyotengeneza itafanya kazi, hivyo kina umuhimu mkubwa. Kinahitaji kufanyiwa kazi vizuri ili biashara iweze kwenda vizuri.

Rafiki, hivyo ndivyo vipengele vitano vya mchanganuo wa biashara ambayo itakuwa na mafanikio makubwa sana kwako.

Kama ulivyoona, aina hii ya mchanganuo hana ule mtiririko rasmi ambao umezoeleka, ambao huwa unatumika pale unapoandaa mchanganuo kwa ajili ya kupata fedha kutoka kwa watu wengine. Na hii ni kwa sababu unapoandaa mchanganuo kwa kutumia vipengele hivi vitano, humwandalii mtu mwingine yeyote bali wewe mwenyewe. Aina hii ya mchanganuo inakuwezesha wewe kuijua vizuri biashara yako na kuweza kuikuza zaidi.

Kwenye makala ya TANO ZA JUMA la 41 la mwaja huu 2019, tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa THIS IS MARKETING. Kupitia kiabu hicho tunakwenda kujifunza njia bora ya kufanya masoko, njia bora ya kutengeneza wateja wanaokutegemea. Kama ambavyo Seth anasema, masoko yanakuwa yamefanikiwa pale watu wanapojiambia; “watu kama sisi huwa wanafanya vitu kama hivi”, hapo unakuwa umetengeneza hadithi ambayo inawavutia wateja kuwa sehemu ya biashara yako.

Ili uweze kusoma makala hiyo pamoja na #MAKINIKIA kutoka kwenye kitabu hicho, hakikisha umejiunga na channel ya TANO ZA JUMA kwenye mtandao wa telegram. Maelezo ya kujiunga na channel hiyo yako hapo chini, yasome na kisha chukua hatua mara moja. Kwa kujiunga unakwenda kupata chambuzi za vitabu mbalimbali pamoja na vitabu vyote vya nyuma vilivyochambuliwa.

#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.

Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.

Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.

Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu

elimu fedha 2