Rafiki, watu wengi wanaoingia kwenye biashara wamekuwa wanashindwa au wanakwamba kutokana na vipaumbele wanavyojiwekea.

Wengi wanaenda kwenye biashara kwa lengo moja, kupata faida. Hivyo wanakazana kufanya vile vitu ambavyo vitaleta faida, tena ya muda mfupi.

Wanaweza kupata faida hiyo kweli, lakini huwa haidumu, biashara inakosa msingi na baadaye kufa au kushindwa kukua.

Pamoja na kwamba unaingia kwenye biashara kupata faida, lakini hiyo pekee haipaswi kuwa kinachokusukuma. Badala yake unapaswa kuwa na kitu kingine muhimu kinachokusukuma ambacho kwa kukijenge msingi mzuri, kitafanya uweze kupata faida.

Eneo muhimu kwako kufanyia kazi kwenye biashara yako ni wateja. Lengo lako kuu linapaswa kuwa kutengeneza wateja ambao wanaitegemea biashara yako, na wateja hawa ndiyo watakaonunua na kuleta faida.

Ukiweka nguvu zako kwenye kutengeneza wateja wazuri wa biashara yako, lengo la faida litafikiwa bila ya tatizo lolote. Lakini kama utaweka nguvu zako kwenye faida tu, hutaweza kutengeneza wateja ambao wataleta faida zaidi.

customer cycle.jpg

Kwa ufupi sana, leo tunakwenda kujifunza hatua kumi za kumnasa mteja kwenye biashara yako na kuwa naye kwa muda mrefu.

Zisome hatua hizi, zielewe, zifanyie kazi kwenye biashara yako na kwa hakika utayaona matokeo mazuri.

Moja; mvutie mteja kwenye biashara yako.

Hii ndiyo hatua ngumu kwa sababu tunaishi kwenye zama za kelele, zama ambazo kila mtu anajitangaza na wateja wamekosa uaminifu kwenye matangazo mbalimbali.

Hivyo wewe chagua njia ya kuwavutia wateja kwenye biashara yako, wale wasiojua uwepo wako wajue na waje kununua kwako.

Kuwa na kitu cha tofauti na kitangaze hicho ili kuwavutia wateja kuja kwako.

Mbili; muuzie mteja.

Kumvutia mteja peke yake haitoshi kumfanya kuwa mteja. Mtu siyo mteja wako mpaka awe ametoa fedha na kununua kitu. Hata kama atakuja kwenye biashara yako na kuulizia au kuahidi kwamba atanunua siku nyingine, huyo bado siyo mteja.

Hivyo unapaswa kuwa na mbinu za mauzo zinazomshawishi mteja kutoa fedha zake na kununua kile unachouza. Hapa unapaswa kumpa mteja manufaa yanayopatikana kwenye kile unachomuuzia na jinsi yanatatua mahitaji aliyonayo.

SOMA; Hivi Ndivyo Vipengele Vitano Vya Mchanganuo Bora Wa Biashara Itakayokupa Mafanikio Makubwa.

Tatu; kusanya mawasiliano ya wateja wako.

Mteja akishanunua kwako, hakikisha unakusanya mawasiliano yake na taarifa zake nyingine. Mteja aliyenunua kwako amekuamini na hivyo unahitaji kuendelea kujenga uaminifu huo ili aendelee kuwa na wewe zaidi. Unahitaji kuendelea kuwasiliana naye kwa njia mbalimbali.

Hivyo hakikisha unakusanya mawasiliano ya wateja wako. Waombe wakupe mawasiliano yao na waeleze utayatumiaje, maana watu hawapendi kusumbuliwa. Waeleze ni kwa manufaa yao ili baadaye kupata taarifa ya vitu vizuri vinavyokuwepo.

Nne; mfanye mteja ajisikie wa kipekee.

Kila mtu anapenda kujisikia wa kipekee, hivyo unapomfanya mteja wako kujisikia wa kipekee, hatokuacha kamwe.

Zipo njia ndogo ndogo na rahisi za kumfanya mteja ajisikie wa kipekee, mfano kumshukuru kwa manunuzi aliyofanya, kumpa zawadi fulani, kumpa upendeleo fulani na kadhalika. Kuna mikahawa ambayo ina vikombe vya kahawa vyenye majina ya wateja, je huoni mteja atajisikia wa kipekee kwenda kupata kahawa hapo?

Tano; boresha mawasiliano na wateja wako.

Baada ya kupata mawasiliano ya wateja wako, wasiliana nao mara kwa mara. Wape taarifa za mali au huduma mpya zinazopatikana, wape taarifa za ofa na zawadi mbalimbali. Pia wape taarifa za matukio mbalimbali yanayohusu biashara yako ambayo yatawanufaisha.

Kumbuka mawasiliano yoyote unayofanya na wateja wako yawe yenye kuwanufaisha na pia yasiwe usumbufu kwao.

Sita; jibu maswali na changamoto za wateja wako.

Wateja watakuwa na maswali mbalimbali kuhusu biashara yako, yajibu vizuri na kwa muda. Wateja watakutana na changamoto mbalimbali kwenye bidhaa au huduma unazowauzia, wasaidie kuzitatua. Kila unapokutana na mteja anayelalamikia chochote kuhusu biashara hiyo, chukua nafasi kumsaidia na atageuka kuwa mteja mwenye furaha na kuiamini biashara yako.

Kuna fursa nyingi za kuwafanya wateja kujisikia vizuri na kupata huduma bora pale wanapokutana na changamoto mbalimbali. Tumia vizuri fursa hizo.

Saba; tengeneza jumuiya ya wateja kujiunga.

Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii, hivyo huwa tunapenda kuwa kwenye jumuiya. Tumia nguvu hii ya jumuiya kuwafanya wateja kuwa nawe kwa muda mrefu. Tengeneza klabu au vikundi ambavyo wateja wako wanaweza kujiunga navyo na wakakutana na wateja wengine na hivyo kujenga ushirikiano.

Kwa zama hizi, ni rahisi kutengeneza vikundi au jumuiya hizi hasa kwa kutumia makundi ya kwenye mitandao ya kijamii.

Nane; waombe wateja kuwaambia watu wao wa karibu.

Kwa kufanyia kazi hatua hizo hapo juu, utakutana na wateja wenye furaha sana, wateja watakuja kwako na shuhuda mbalimbali jinsi biashara yako imewasaidia. Na unapokutana na wateja wa aina hii ombi lako linapaswa kuwa moja, waombe wakupe wateja zaidi. Waombe wateja wako wawaambie watu wao wa karibu nao waje kunufaika kwenye biashara yako.

Wateja wanaoletwa na wateja walioridhika huwa ni wateja wazuri kuliko wale wanaoletwa na matangazo mbalimbali. Hivyo tumia wateja ulionao sasa kutengeneza wateja zaidi kwenye biashara yako.

SOMA; Siri 101 Za Mafanikio Kwenye Biashara Ambazo Hazifundishwi Popote Pale.

Tisa; endelea kumuuzia mteja zaidi.

Mteja akinunua kwako mara moja halafu asirudi tena, ni hasara kwa biashara yako. Unafaidika na mteja pale anaponunua tena na tena na tena. Hivyo washawishi wateja wako kurudi kununua kwako tena.

Kwa kufanyia kazi hatua zote hapo juu, unamfanya mteja kuendelea kuwa na biashara yako.

Kumi; rudia mzunguko huo.

Ukishachukua hatua hizo tisa kwa mteja mmoja, rudia tena kwa mteja mwingine na mwingine na mwingine. Kwa kifupi hili ndiyo linakuwa jukumu lako kuu kwenye biashara, kuvutia mteja na kumfanya aendelee kukaa na wewe kwa kumpa manufaa na kuwa na mawasiliano bora naye.

Hizo ndiyo hatua kumi za kumnasa mteja na kuwa naye kwenye biashara yako kwa muda mrefu na hivyo kuweza kujenga biashara yenye msingi sahihi na itakayofanikiwa sasa. Weka hatua hizi kwenye matendo kwa biashara ya aina yoyote ile unayofanya na utaweza kunufaika sana.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania