Kuna saa inauzwa shilingi elfu moja, nyingine inauzwa shilingi laki moja na nyingine inauzwa shilingi milioni moja. Swali ni je kati ya saa hizo tatu, ni ipo inatoa majira sahihi ya muda?

Jibu ni zote zinatoa majira sahihi ya muda, bila ya kujali inauzwa kwa bei gani.

Sasa swali linakuja, kwa nini saa ambazo zote zinatoa majira kwa usahihi zitofautiane bei kwa kiasi kikubwa hivyo?

Unaweza kukimbilia kusema tofauti ni kwenye ubora, kwamba saa ya shilingi milioni moja ni bora kuliko ya shilingi elfu moja. Na hilo halina ubishi. Lakini kweli unataka kuniambia ubora pekee ulete tofauti kubwa kiasi hicho? Jibu ni hapana, kuna zaidi ya ubora.

Na kitu hicho cha ziada ni hadhi (status). Sisi binadamu huwa tunapima umuhimu wetu kwenye jamii kupitia hadhi tuliyonayo. Wale wa hadhi ya juu wanaonekana kuwa muhimu zaidi kuliko wa hadhi ya chini.

Sasa, moja ya vitu ambavyo vinaweza kuonesha hadhi ya mtu, ni vitu anavyomiliki. Kama kuna watu wawili, mmoja amevaa saa ya shilingi elfu moja na mwingine amevaa saa ya milioni moja, mwenye saa ya milioni moja anaonekana kuwa na hadhi ya juu kuliko mwenye saa ya elfu moja.

Ukiondoa yale mahitaji ya msingi kabisa, yaani chakula, malazi na mavazi, vitu vingine vyote tunavyonunua ni kwa ajili ya hadhi. Mtu ananunua kitu chochote cha bei ghali, siyo kwa sababu kitu hicho ndiyo sahihi kuliko vitu vingine, bali kwa sababu kitu hicho kinampa hadhi ya juu zaidi kwenye jamii yake.

Hivyo unaweza kulitumia hili vizuri kama unafanya biashara, kwa kuwaonesha wateja wako jinsi ambavyo hadhi yao itaongezeka pale watakaponunua unachouza, au itashuka kama hawatanunua.

Lakini pia, unaweza kulitumia kuacha kuwa mtumwa wa hadhi, kwa kujiamini kwamba umekamilika na huhitaji kupandisha hadhi yako kwa vitu vya nje. Hii itakusaidia sana pale unapoanzia chini na unajijenga kimafanikio. Badala ya kununua vitu vya maonesho, unawekeza fedha zako kwenye kitu kinachoweza kuzalisha zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha