“There’s nothing worse than a wolf befriending sheep. Avoid false friendship at all costs. If you are good, straightforward, and well meaning it should show in your eyes and not escape notice.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 11.15

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ambayo tumeiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kupata matokeo makubwa.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari URAFIKI WA UONGO…
Hakuna kitu kibaya kama urafiki wa uongo, mtu unayejua ni rafiki yako na unaweza kumtegemea wakati wa uhitaji, lakini anageuka kuwa adui mkubwa kwako.
Hawa ni mbwa mwitu ambao wamejivika ngozi ya kondoo.
Wakiwa na wewe wanaonekana wako upande wako, lakini wakiwa mbali wanakusema vibaya.
Hawa ni marafiki ambao mambo yako yakiwa vizuri wanakuwa na wewe, lakini mambo yakienda vibaya huwaoni.
Sifa zao ni watu wenye wivu, wasiojali, na wabinafsi.
Wakati mwingine wanakushauri vibaya ili ushindwe au uanguke na wao wafurahie.
Ni wajibu wako kuwaangalia vizuri wale unaowaita marafiki zako, na kujua ni wapi marafiki wa kweli na wapi ni ‘washikaji’ tu.
Rafiki wa kweli ni yule ambaye yupo tayari kufanya chochote kwa ajili yako, yupo tayari kupoteza kukusaidia wewe unapokuwa na uhitaji na matatizo yako yanakuwa yake, atakuwa tayari kukutetea hata kama haupo mahali fulani ambapo wengine wanakusema vibaya.
Washikaji ni wale marafiki ambao mnakutana pamoja kwa kitu fulani pekee, labda kazi, biashara, starehe n.k. Lakini baada ya hapo kila mtu anaenda na mambo yake.

Kwa upande wa pili, hakikisha na wewe unakuwa rafiki wa kweli kwa wale marafiki zako.
Usiwe rafiki wa uongo, rafiki wa mashaka, rafiki wa mambo yanapokuwa mazuri.
Chagua wale marafiki ambao ni wa kweli kwako na wewe kuwa wa kweli kwao.
Marafiki wa aina hii hawawezi kuwa wengi, hivyo unapowapata ni vyema kuboresha mahusiano hayo kwa kuwa yanakuwa na manufaa makubwa kwa kila mmoja.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwatambua marafiki wa kweli kwako na wewe kuwa wa kweli kwao, siku ya kuwajua marafiki wote wa uongo na kuwaweka kwenye kundi sahihi ili usije kuumia pale unapowategemea na wao kukuangusha.
#TengenezaUrafikiMzuri #JitoeKwaAjiliYaWengine #WatambueMarafikiZakoWaKweli

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1