Sisi binadamu ni viumbe ambao tuna ubinafsi mkubwa.
Huwa tunayaangalia maslahi yetu kwanza kabla hatujasumbuka na mambo mengine.
Na hili la kuangalia maslahi yetu kwanza, limetumika vizuri na wengine katika kupata kile wanachotaka kupata kutoka kwetu.
Tupo tayari kulipa zaidi kwenye kitu chochote, pale kinapokuwa na sifa zifuatazo;
- Ni kitu cha kipekee, ambacho hatuwezi kukipata sehemu nyingine yeyote.
- Tuna uhitaji wa haraka na hatuna muda wa kuendelea kusubiri.
- Tunafikiri thamani yake itakua zaidi ya ilivyo sasa.
- Kwa sababu ndiyo chaguo pekee linalotufaa katika machaguo machache yaliyopo.
- Kwa sababu kuna uhaba wa kitu hicho, hivyo tusipolipia zaidi hatutakipata kabisa.
Katika hali hizo tano, hata mtu ambaye ni bahili kiasi gani, atakuwa tayari kulipa zaidi kwa kile ambacho amekipata, kwa sababu asipochukua hatua sasa, atakikosa kabisa.
Watu wamekuwa wanatengeneza njia hizo ili kukusukuma wewe kulipa zaidi. Wanakutengenezea mazingira ya kitu kuwa kwa uhaba na upekee ili usukumwe kuchukua hatua sasa na usikikose.
Na wewe pia unaweza kuongeza thamani ya chochote unachokifanya, kama utazingatia vitu hivyo vitano; kifanye kwa utofauti, wafikie wenye uhitaji wa haraka, toa thamani kubwa zaidi na weka uhaba wa kiwango au muda wa upatikanaji wake.
Unastahili kulipwa zaidi ya unavyolipwa sasa, anza kwa kutengeneza mazingira sahihi yatakayowapelekea watu kuwa tayari kukulipa zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,