Kila ninapokutana na watu ambao wanasema majukumu yao ya kazi ni mengi na hivyo wanakosa muda wa kufanya vitu vingine muhimu kwenye maisha yao, huwa kuna kitu kimoja kinakuwa nyuma yao, wanakuwa wanategemewa zaidi na wengine.
Watu wengi huwa wanatumia muda wao wa kazi kujibu na kusaidia wengine kukamilisha majukumu yao, kitu ambacho kinawanyima wao muda wa kufanya yale muhimu. Kinachotokea ni siku ya kazi inaisha, mtu hajakamilisha majukumu yake na inambidi afanye kazi muda wa ziada, au aende na kazi nyumbani.
Mara nyingi unakuta mtu huyo ana ujuzi ambao wengine hawana au anaweza kufanya kitu ambacho wengine hawataki kufanya. Hivyo wengine wanapokwama kwenye kitu fulani, wanaenda kwa mtu huyo kusaidiwa kukifanya.
Sasa kama wewe ni mtu ambaye kazini kwako watu wanakutegemea wewe pale wanapokwama, au kwenye biashara yako vitu vingi haviwezi kufanyika kama wewe haupo, basi kuna tatizo kubwa, na usipolifanyia hili kazi hutaweza kutoka pale ulipokwama sasa.
Najua kuna kaufahari fulani mtu unakapata pale wengine wanapokutegemea wewe wanapokwama, lakini unachopaswa kujua ni kwamba huo ni mzigo mkubwa zaidi kwako.
Watu wakishajua yupo mtu ambaye atawasaidia kila wanapokwama, hicho ndiyo kitu ambacho watakifanya kila mara. Hata kwa jambo dogo ambalo wangeweza kujifunza na kulifanyia kazi, hawatafanya hivyo kama wanajua wewe upo tayari kuwasaidia pale walipokwama.
Sasa ufanye nini ili kuondoka kwenye tatizo hili?
Yapo mengi ya kufanya, ila anza na haya mara moja.
- Pale mtu anapokuja kwako na tatizo alilokwama na anataka umsaidie, hapo hapo mwelekezi jinsi ambavyo anaweza kulitatua mwenyewe wakati mwingine na siyo kukutegemea wewe. Usifanye wewe, mwelekeze jinsi ya kufanya mwenyewe na atajifunza vizuri zaidi.
- Weka muda maalumu wa kuwahudumia wengine wanaohitaji msaada wako. Isiwe kila dakika mtu akikwama jambo anakuja kwako, hivyo hutaweza kufanya kazi. Tenga muda wa kazi ambao hutaruhusu usumbufu wa aina hiyo kabisa, labda kama ni dharura kubwa.
- Angalia maeneo ambayo wengi wanakwama na kuhitaji msaada wako, kishatengeneza mwongozo mfupi na wapatie watu wote. Mwongozo huo uwe unaeleza jinsi ya kutatua changamoto ambazo watu wanakutana nazo.
- Kama wewe ni bosi au unamiliki biashara na umeajiri, hakikisha kila aliye chini yako anayaua majukumu yake na anaweza kuyatekeleza kwa usahihi. Hii itapunguza hali ya kuwasumbua wengine pale wanapokwama.
- Kuwe na mawasiliano ya mara kwa mara baina ya watu wote wanaofanya kazi kwenye idara moja, mfano mikutano ya kabla ya kuanza kazi. Hapo changamoto mbalimbali zinajadiliwa na pia inaweza kuwa nafasi ya kuelekezana kwa wale wanaokutana na changamoto mbalimbali.
Usikubali watu wajenge tabia ya kutua mizigo yao kwako kwa sababu wewe ndiye unayejua kile wanachokwama. Kila mtu anaweza kuelekezwa na akajua, fanya hivyo ili uweze kupata muda zaidi wa kufanya kazi zako na siyo kuwa unazima moto muda wote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,