‘Nataka kuibadili dunia…’

Ni kauli maarufu kwa wengi, huwa tunajiwekea lengo kubwa kiasi hicho kupitia chochote tunachofanya, na kufikiria tunaweza kuwa na mchango mkubwa hapa duniani kama tutaweza kuibadili.

Lakini hilo ni lengo ambalo siyo tu hatuwezi kulifikia, bali pia tunajidanganya, kwa sababu ni kitu ambacho kipo nje ya uwezo wetu kabisa. Na kadiri tunavyokazana kulitimiza, ndivyo tunavyokutana na vikwazo na kushindwa.

Hata kwa kujiuliza tu, unaposema unataka kuibadili dunia unamaanisha nini hasa? Yaani jinsi hii dunia ilivyo, kipi hasa unafikiri utakibadili kutoka kilivyo sasa na kuwa unavyofikiri ni sahihi? Na unawezaje kufanya hivyo?

Unapojiuliza maswali hayo na kufikiri kwa kina, unagundua kwamba kuibadili dunia siyo kitu rahisi kama wengi wanavyosema. Lakini pia kushindwa kuibadili dunia hakupaswi kutukatisha tamaa na kuona maisha yetu hayana maana.

Kwani yapo mambo mengi sana unayoweza kuyafanya, japo hayataibadili dunia, lakini yatakuwa na mchango kwenye kuifanya dunia iwe bora zaidi ya ilivyo sasa.

Na moja ya mambo muhimu sana unayoweza kufanya na ukachangia dunia kuwa bora ni kufanya kile kilicho sahihi mara zote. Kwenye kila unachofanya na kila hali unayopitia, huwa kuna machaguo mawili, kufanya kilicho sahihi (ambacho huwa siyo rahisi) na kufanya kilicho rahisi.

Wengi kwa kutokupenda ugumu, huwa wanakimbilia kufanya kilicho rahisi, na mara zote kilicho rahisi huwa siyo kilicho sahihi.

Sasa kama wewe utaondoka kwenye huo mkumbo wa kufanya kilicho rahisi na chenye madhara, na kuchagua kufanya kilicho sahihi japo ni kigumu, kuna alama fulani utakayoiacha hapa duniani, na utakuwa na mchango bora sana kwa wengine pia.

Kila unachofanya ni muhimu kuliko matokeo utakayopata, weka nguvu na juhudi zako kwenye kufanya kilicho sahihi, na usihangaike sana na matokeo utakayopata. Kwa sababu unachoweza kudhibiti wewe ni kile unachofanya na siyo matokeo.

Ndiyo maana huwezi kuibadili dunia, kwa sababu kuibadili dunia ni matokeo, kitu ambacho kipo nje ya uwezo wako. Lakini unaweza kuchagua leo na kila siku kufanya kile kilicho sahihi, ambayo ipo ndani ya uwezo wako. Na kwa kufanya kilicho sahihi, huenda ukaleta mchango fulani kwa dunia na wengine, lakini hicho siyo kinachokusukuma kufanya.

Unasukumwa kufanya kilicho sahihi mara zote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha