“Crimes often return to their teacher.”
—SENECA, THYESTES, 311
Kupata nafasi hii nzuri ya kuiona siku ya leo ni bahati ya kipekee sana kwetu.
Siyo kwa sababu tunastahili sana au kwa sababu ya juhudi zetu, bali ni bahati tu.
Kazi yetu hapa duniani bado haijakamilika, hivyo leo tuna nafasi nyingine ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UNACHOWAFUNDISHA WENGINE, KITARUDI KWAKO…
Chochote kibaya unachowafundisha wengine kufanya, kuna siku kitarudi kwako, kuna siku watakufanyia ubaya huo na wewe pia.
Kama una biashara na unawafundisha wafanyakazi wako jinsi ya kuwaibia wateja, kuna na uhakika kuna siku wafanyakazi hao hao watakuibia na wewe pia.
Kama ni watoto wako umewafundisha jinsi ya kudanganya ili kukwepa majukumu kuna siku watakudanganya wewe na kuyakimbia majukumu yao kwako.
Kama utawafundisha wengine jinsi ya kuwa waonevu, kuna siku watakuonea na wewe pia.
Ubaya na uovu wowote unaowafundisha watu wengine kufanya, kuna siku watakufanyia uovu huo wewe pia.
Ni kanuni ya asili, ndivyo dunia inavyokwenda.
Wapo wanaosema malipo ya kila kitu yako hapa hapa duniani,
Na wengine wanasema unachowafanyia wengine ndiyo utakachofanyiwa.
Vyovyote unavyoamini, lakini kuwa na uhakika, hakuna utakachofanya na ukaondoka bila kupata malipo yake.
Fanya wema na utalipwa wema, fanya ubaya na utalipwa ubaya.
Unapoona unafululiza kulipwa ubaya, kabla hujaanza kulaumu watu, hebu angalia ni vitu gani ulifanya huko nyuma.
Utaona jinsi ambavyo wewe mwenyewe uliwatengeneza wale wanaokufanyia ubaya sasa.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuepuka kufanya ubaya au kuwafundisha wengine kufanya ubaya kwa sababu mwisho wa siku ubaya huo utarudi kwako mwenyewe.
#UnavunaUlichopanda #MalipoNiHapaHapa #AsiliHaikopwi
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1
Kweli kabisa Kocha,malipo ni hapa hapa duniani.
swali,Kama nimewahi kufanya ubaya,na nikagundua kuwa nilikosea na nikakili makosa yangu kwa kujilekebisha.Je? naweza kuondolewa hayo malipo ya ubaya..?
Ahsante.
LikeLike
Kinachosaidia pale unapotambua ulifanya kosa huko nyuma na kujirekebisha ni kwamba malipo yatakapokuja utajua kabisa yametokana na nini na pia hutatengeneza makosa mengine mapya.
Lakini kile ambacho tayari umeshakipanda, lazima utakivuna kwa namna moja au nyingine.
Asili huwa haikopwi.
LikeLike
Ni kweli kocha, malipo ni hapa hapa duniani.
Kuna wakati nilikuwa na tabia ya kuchukua kazi watu Wengine na kuanza kuzisambaza kama Mimi ndiyo nimeziandaa lakini baadae nikakiri makosa yangu kuomba radhi Kwa wale niliokuwa nawafanyia hayo. Nikasamehewa na maisha yakaendelea. Mwaka mmoja baadae nikawa nimeanza kazi za uandishi, kuna watu wanaiba kazi zile na kuanza kuzisambaza kama zao. Malipo ni hapa hapa duniani, nimepokea malipo yangu.
LikeLike
Vizuri Tumaini kwa kujifunza kwa njia ya maumivu,
Ni rahisi sana kuwafanyia wengine kitu fulani, lakini kitu hicho hicho kinapofanywa kwako, maumivu yanakuwa makubwa.
Tunapopata nafasi hizi za kujifunza, tuzitumie kuhakikisha tunakuwa bora zaidi.
LikeLike