Ipo kauli moja ya utani kwamba pale Mungu anapotaka kutuadhibu, huwa anatupa kila tunachotaka.

Kauli hiyo siyo tu ya utani, bali imebeba ukweli mkubwa sana kuhusu maisha.

Unaweza kuona maisha yako hayajakamilika kwa sababu kuna vitu unataka lakini bado hujavipata, lakini hilo lina manufaa kwako. Kwa kukosa baadhi ya vitu unavyotaka, kunakusukuma kuendelea kuchukua hatua kila siku na kuwa bora zaidi.

Lakini kama utapata kila unachotaka, unakuwa huna tena kinachokusukuma kuchukua hatua na kuwa bora zaidi. Unajikuta upo upo tu na unaishia kufanya mambo ambayo yana madhara makubwa kwako.

Kudhibitisha hili angalia watu wengi wanaokutana na bahati fulani kwenye maisha na kupata kila wanachotaka. Angalia watu wanaoshinda bahati nasibu wanaorithi mali na wengine wanaokutana na bahati ya kupata fedha nyingi kwa wakati mmoja. Wanajikuta kwenye nafasi ya kuweza kupata chochote wanachotaka bila ya kusumbuka, na hili hupelekea maisha yao kuharibika zaidi.

Kama unataka kuwa na maisha bora wakati wote, kama kila wakati unataka kuwa kwenye njia sahihi ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa na kubaki kwenye mafanikio hayo, hakikisha kila wakati kuna kitu unachotaka ambacho bado hujakipata. Hivyo anza kwa kujiwekea malengo makubwa mno, malengo ambayo wewe mwenyewe unaona huwezi kuyafikia, lakini amini utayafikia na weka juhudi zako kwenye kuyafikia.

Utakapoyafikia malengo hayo makubwa uliyojiwekea, weka tena lengo kubwa zaidi, mara kumi ya lengo la kwanza na anza kufanyia kazi. Ukienda kwa njia hii, kila wakati unakuwa na kitu cha kukusukuma kuwa bora zaidi na hivyo kujiondoa kwenye hatari ya kufanya mambo yanayokuharibu zaidi pale unapokuwa umeshapata kila unachotaka.

Usiumie pale ambapo hujapata kila unachotaka, bali jua nini umekosa na weka juhudi zako kwenye kukipata, na ukishakipata, weka lengo la kingine kikubwa zaidi. Hapa siyo kwamba huridhiki na maisha yako, bali unajizuia usiwe na muda wa kufanya mambo yatakayokupoteza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha