Wazo bora ni kama mvinyo, kadiri muda unavyokwenda, ndivyo mvinyo unavyokomaa na kuwa bora zaidi.

Wazo bora pia ni kama uwekezaji, kadiri muda unavyokwenda ndivyo uwekezaji unakua thamani.

Usitegemee kupata wazo siku moja, kuchukua hatua halafu kupata matokeo makubwa unayotarajia. Mafanikio huwa hayaendi hivyo.

Unapata wazo ambalo unaamini ni bora sana, moja kwa moja unakwenda kuchukua hatua kwenye wazo hilo na unaanza kugundua kuna madhaifu mengi kwenye wazo hilo. Unagundua kuna vitu vingi hukuwa umevifikiria hapo kabla. Na hapa ndipo wengi hukata tamaa na kuona wazo walilonalo halifai.

Kukata tamaa kwenye wazo jipya uliloanza kulifanyia kazi ni kosa kubwa sana unaloweza kufanya kwenye maisha yako.

Kwa wazo lolote unalopata, jua halijakamilika, jua linahitaji kuchukua hatua na muda wa kulikomaza ili liwe bora na kuzalisha matokeo unayoyatarajia.

Hivyo anza na wazo lako na unapokutana na changamoto, usikimbie, badala yake boresha zaidi wazo hilo, kadiri unavyokwenda ukiboresha, ndivyo wazo hilo linazidi kuwa bora zaidi.

Watu wote waliofanikiwa sana, biashara zote kubwa unazozijua, watu hawakuanza na mawazo hayo mwanzoni, walianza na wazo jingine kabisa, lakini walipoingia kwenye kufanya, wakagundua mawazo waliyokuwa nayo hayakuwa sahihi. Hivyo wakaendelea kuboresha mpaka wamefika pale walipo sasa.

Kuwa mvumilivu, kuwa na subira, kuwa mtu wa kuchukua hatua za kuboresha kila wakati na utaweza kutengeneza wazo bora sana kwako na litakalokuwezesha kufikia mafanikio makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha