Maisha ni magumu, lakini kuna wakati huwa tunayafanya yawe magumu kuliko yanavyopaswa kuwa.
Na tumekuwa tunafanya hivyo kupitia kujibebesha mizigo isiyo kuwa na maana wala manufaa yoyote kwetu.
Kwa asili, kitu chochote kisichokuwa na matumizi kwenye mwili huwa kinaondolewa. Ndiyo maana utakula chakula ambacho ni kitabu mno, ambacho huenda umekigharamia kwa kiasi kikubwa cha fedha. Lakini sehemu ndogo tu ya chakula hicho ndiyo itachukuliwa na mwili, nyingine inabaki kama kinyesi na inapaswa kuondolewa mwilini. Iwapo kinyesi hicho hakitaondolewa, basi mwili utatengeneza matatizo makubwa sana.
Hivi ndivyo kila eneo la maisha yetu lilivyo, tunapong’ang’ana na vitu ambavyo tunapaswa kuvitoa, tunatengeneza matatizo makubwa sana.
Unapobeba vinyongo ambavyo ulipaswa kuachana navyo zamani na kusonga mbele, unaharibu sana mahusiano yako na wengine na hata kuvuruga utulivu wako wa ndani.
Unapobeba hasira zisizo na umuhimu, unaharibu utulivu wako na hata kujizuia kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.
Unapobeba uzito uliopitiliza kwenye mwili wako, unakaribisha magonjwa sugu na yasiyotibika kama kisukari, presha, kansa na mengineyo.
Unapong’ang’ana na mahusiano yasiyo na tija kwako, unajiweka kwenye nafasi ya kunyanyasika, na pia kujikosesha mahusiano ambayo ni bora kwako.
Unapong’ang’ana na kazi ambayo huipendi na haikulipi, unajizuia kupata fursa kubwa na zitakazokuwezesha kupiga hatua zaidi.
Kwa tulio wengi, huwa tunaianza siku kwa kupunguza mzigo wa chakula ambacho hakijatumika (kinyesi). Napendekeza tutumie muda huo huo kutafakari mizigo mingine tuliyoibeba kwenye maisha yetu na kuitua pia.
Kama ambavyo tunatoka kwenye zoezi hilo tukijisikia wepesi tumboni, basi pia tutoke tukijisikia wepesi akilini na rohoni pia. Using’ang’ane na chochote ambacho hakina manufaa kwako, kitakutengenezea matatizo yatakayokukwamisha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,