“Don’t seek for everything to happen as you wish it would, but rather wish that everything happens as it actually will—then your life will flow well.”
—EPICTETUS, ENCHIRIDION, 8
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ambayo tumeiona leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KUBALIANA NA MATOKEO…
Huwa tunapenda kila kitu kiende kama tulivyopanga sisi, tupate yale matokeo ambayo tumepanga kupata.
Na mambo yanapokwenda tofauti na tulivyotegemea, tunakasirika, tunapata msongo, tunaona hatuna bahati na mengine mengi ya kutuvuruga.
Lakini tunajua wazi kwamba matokeo tunayoweza kupata hayapo ndani ya uwezo wetu,
Hatua tunazochukua zipo ndani ya uwezo wetu, lakini matokeo tunayopata hayapo ndani ya uwezo wetu kabisa.
Tunaweza kufanya kila tunachopaswa kufanya, lakini matokeo yakaja tofauti kabisa.
Hivyo tunapaswa kukubaliana na matokeo tunayopata, iwe ni mazuri au mabaya, na kisha kuchukua hatua sahihi kulingana na matokeo hayo
Usijiambie kama matokeo yangekuja hivi basi mambo yangekuwa mazuri.
Badala yake jiambia sasa matokeo yamekuja hivi, ni jukumu langu kuyatumia kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri.
Kukubali matokeo unayopata pekee haitoshi, bali pia unapaswa kuyapenda.
Yapende matokeo unayopata, hata kama siyo uliyotegemea na utakuwa tulivu pamoja na kuweza kuchukua hatua sahihi kwenye matokeo hayo.
Tukazane na kile kilicho ndani ya uwezo wetu na tukubaliane na kile kilicho nje ya uwezo wetu.
Haimaanishi kwamba tutakubaliana na uzembe wetu wenyewe au wengine, bali unahakikisha upande wako uko sahihi, umefanya kila ulichopaswa kufanya na kwa namna unayopaswa kufanya.
Kisha matokeo yoyote unayoyapata, unayapokea, unakubaliana nayo na unayapenda ili kuweza kusonga mbele zaidi.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuweka juhudi kwenye hatua unazochukua, lakini kuwa tayari kupokea na kupenda matokeo yoyote utakayopata, hata kama siyo yale uliyotegemea kupata. Maana juhudi zipo ndani ya uwezo wako na matokeo yako nje ya uwezo wake.
#KubalianaNaMatokeo #HangaikaNaYaliyoNdaniYaUwezoWako #TumiaMatokeoUnayopataKusongaMbeleZaidi
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1