Mtu mmoja mwenye busara amewahi kusema maneno haya; “katika watu 100 wanaoweza kuongea, ni mmoja pekee anayeweza kufikiri, katika watu 1000 wanaoweza kufikiri, ni mmoja pekee anayeweza kuona”.

Ni kauli ngumu na tata ambayo huwezi kuielewa kwa sababu ya alichokieleza mtu huyo.

Kwa kifupi ni kwamba kila mtu anaweza kuongea, na hivi mawasiliano yamerahisishwa, kila mtu ni mwongeaji, wengi ni waropokaji na wanaongea mambo ambayo baadaye yanakuja kuwasumbua. Lakini ni wachache sana wanaofikiri kabla ya kuongea. Wachache sana wanaotafakari kwa kina kabla hawajasema walichonacho, na hawa ndiyo tunawaona wana busara.

Lakini katika hao wachache wanaofikiri kabla hawajaongea, kuna wachache zaidi ambao wanaweza kuona. Watu wengi hawaoni, kuna vitu vingi vizuri ambavyo vimewazunguka watu, lakini wamekuwa hawavioni. Siyo kwa sababu wana upofu, bali kwa sababu hawana maono. Macho yanaona kile ambacho tayari unakijua, usichokujua hayawezi kuona. Lakini mtu anapokua na maono makubwa, kuwa na picha kubwa ambayo bado hajaifikia, macho yake yanafunguka zaidi na anaziona fursa ambazo wengine hawazioni.

Kama unataka kuwa mbobezi, kama unataka mafanikio makubwa. Lazima uwe kati ya wachache wanaoweza kuongea, kufikiri na kuona. Hapo utaweza kugeuza mazingira yoyote na yakawa bora sana kwako na wewe kupata chochote unachotaka. Haihitaji akili nyingi wala elimu kubwa kuweza kutekeleza hili, bali inahitaji uwe tayari kujitoa kusikiliza, kudadisi na kuwa na maono makubwa.

Anza kuona visivyoonekana, fikiri kwa umakini kabla hata hujaongea na kila wakati utaongea kilicho sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha