Watu wengine wanapokuwa na matatizo ni rahisi kuwafariji na kuwashauri kwamba wasijali mambo yatakwenda vizuri.

Ila sisi wenyewe tunavyokuwa na tatizo kama hilo hilo, huwa tunaona kwetu ni la tofauti na hivyo ushauri kama ambao tulikuwa tunawapa wenzetu kwetu haufai.

Hiyo ni kujidanganya.

Hakuna tatizo jipya hapa duniani, matatizo ni yale yale tangu enzi na enzi, sema yamekuwa yanakuja kwa njia mpya, kulingana na mabadiliko yanayoendelea kwenye dunia.

Kwa mfano, sasa hivi muda ni tatizo kwa wengi, na tunaweza kusema ujio wa simu na mitandao ya kijamii ndiyo imekuza tatizo hili. Lakini tutakuwa tunajidanganya, watu wamekuwa wanalalamikia muda tangu enzi na enzi.

Miaka 2000 iliyopita, wakati huo hata hakukuwa na magari hivyo watu hawakuwa na mengi ya kufanya, bado watu walikuwa wanalalamika kwamba hawana muda, na mwingi walikuwa wanaupoteza kwenye mambo yasiyo na maana.

Sasa kujua hili kunakusaidia nini?

Kwanza kunakusaidia kujua kwamba utakutana na matatizo hapa duniani, kwa sababu yapo, na hayaendi popote bali kwetu sisi wenyewe.

Pili unapokutana na tatizo usipate taharuki na kuona ni kitu kikubwa ambacho hukiwezi, watu wamekuwa wanasumbuka na tatizo kama hilo kwa miaka mingi sasa.

Tatu inatupa nafasi ya kujifunza kwa wengine, kwa sababu tatizo siyo jipya, basi kuna watu watakuwa wameandika au kufundisha kuhusu tatizo hilo. Hivyo ukitafuta hilo, utalipata na litakuwa na manufaa kwako.

Ni tatizo lipi linakusumbua kwa sasa?

Anza kwa kujiambia siyo tatizo jipya, kisha tafuta maarifa, wengine waliopitia tatizo kama hilo walifanya nini, fanya kama wao na utaweza kupiga hatua zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha