Nimeshaliandika hili mara nyingi mpaka kitabu kizima nimeandika kuhusu muda. Lakini naomba nilirudie tena kwa msisitizo mkubwa.
Hakuna siku hata moja utapata muda wa kufanya kile unachojiambia ukipata muda utafanya.
Kama kuna kitu unajiambia unataka kufanya, lakini kwa sasa huna muda, jua hakuna siku utakuja kupata muda wa kufanya kitu hicho. Hii ni kwa sababu hakuna muda ambao umekaa mahali na unakusubiri wewe uupate. Bali muda pekee ulionao ni huo unaoutumia sasa kwa mambo mengine.
Hivyo kama unataka kupata muda wa kufanya kitu, ni lazima uutengeneze kutoka kwenye muda ulionao sasa. Ni lazima useme hapana kwa baadhi ya vitu unavyofanya sasa, ili uweze kupata muda wa kufanya kile ambacho ni muhimu zaidi kwako.
Kama unajiambia kuna kitu unataka kufanya lakini huna muda, maana yake unasema kitu hicho siyo muhimu kama vile vitu ambavyo unafanya sasa.
Kwa mfano kama unapata muda wa kuzurura kwenye mitandao ya kijamii, kufuatilia maisha ya wengine na habari mbalimbali, lakini huna muwa wa kuanzisha na kukuza zaidi biashara yako, maana yake unasema hayo unayofanya sasa ni muhimu kuliko biashara.
Unaweza kujidanganya utakavyo, lakini matumizi yako ya muda yatakuumbua. Kwa sababu chochote ambacho unakipa muda wako, umekubali kwamba ni muhimu kuliko vile ambavyo umevinyima muda.
Hivyo basi, unapokuwa na kitu muhimu cha kufanya, lakini unaona huna muda, kaa chini na orodhesha vitu vyote ambavyo huwa unafanya kwenye siku yako, kisha linganisha umuhimu wa kila unachofanya na kile ambacho umekosa muda wa kufanya. Kama kuna vitu unafanya sasa ambavyo havina umuhimu mkubwa, achana navyo mara moja na utapata muda wa kutosha kufanya kile ambacho ni muhimu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,