“Think by way of example on the times of Vespasian, and you’ll see all these things: marrying, raising children, falling ill, dying, wars, holiday feasts, commerce, farming, flattering, pretending, suspecting, scheming, praying that others die, grumbling over one’s lot, falling in love, amassing fortunes, lusting after office and power. Now that life of theirs is dead and gone . . . the times of Trajan, again the same . . .”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 4.32

Kuiona siku hii nyingine nzuri ya leo ni bahati kubwa sana kwetu.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.

Asubuhi ya leo tutafakari MAMBO NI HAYA HAYA…
Vizazi vingi vimepita hapa duniani, lakini mambo ambayo vizazi vyote vimekuwa vinafanya ni yale yale.
Watu wamekuwa wanazaliwa, wanakua, wanaoa au kuolewa, wanapata watoto, wanaumwa, wanakufa, wanacheka, wanalia, wanaona wivu, wanaweka vinyongo, wanalima, wanafanya biashara, wanafanya kazi na mlolongo unaendelea.
Hakuna kitu kipya ambacho tunawexa kusema tunakifanya sisi, ila tunaweza kusema tunafanya mambo yake yale kwa njia ambazo ni mpya.

Ni muhimu kutafakari na kuelewa hili kwa sababu kuna watu wamekuwa wanaeneza habari za hofu kwamba dunia imefika mwisho au mambo yanayotokea sasa ni makubwa na mabaya mno.
Wote huo ni uongo, dunia imekuwepo kwa muda mrefu na itaendelea kuwepo, sisi binadamu ndiyo tunaopita, kama walivyopita binadamu wenzetu wengi tangu enzi na enzi.
Na kuhusu mabaya, kuna nyakati dunia imepitia mambo mabaya lakini imedumu. Fikiria majanga makubwa ya asili kama tetemeko la ardhi, mafuriko, vimbunga na kadhalika. Fikiria vita kubwa na mbaya kama vita ya kwanza na ya pili ya dunia.
Pamoja na mambo hayo mabaya na magumu, dunia imeendelea kuwepo.
Hivyo chochote kinachotokea sasa, tujua siyo kipya, huenda tu kimekuja kwa namna mpya.
Na hii dunia tumeikuta na tutaiacha, hivyo tuwe wanyenyekevu na kutumia nafasi hii tuliyoipata vizuri.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutambua kwamba mambo yanayitokea ni yale yale, hakuna jipya hapa duniani. Na dunia itaendelea kuwepo, ila sisi binadamu ndiyo tunaopita.
#HakunaJipya #BinadamuTunapita #DuniaItadumu

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1