Kila mtu huwa anashindwa kwenye maisha, kwenye vitu fulani anavyofanya.
Hata kama mtu ana mafanikio au mamlaka kiasi gani, kuna mambo mengi anaweza kupanga na yasitokee kama alivyopanga, licha ya kuweka kila juhudi anayopaswa kuweka.
Hivyo swali la wewe siyo kujiuliza kama utashindwa au la, bali kujiuliza umefanya nini baada ya kushindwa.
Kwa sababu wale ambao hawafanikiwi kwenye maisha ni wale ambao wakishindwa wanabaki chini na kutumia kushindwa kwao kama sababu ya kutokufanikiwa.
Lakini wale wanaofanikiwa kwenye maisha, ni wale ambao huwa wanainuka tena baada ya kushindwa na kuendelea na mapambano. Wanaweza kushindwa tena, lakini wanainuka tena. Wanakwenda hivyo mpaka pale wanapopata kile wanachotaka.
Rafiki, najua somo hili la kuhusu kushindwa nimeshakuandikia mara nyingi sana, lakini utaona linajirudia kila mara, kwa sababu ni muhimu mno katika kipindi hiki kuliko kipindi kingine chochote.
Tunaishi kwenye kipindi ambacho hadithi za mafanikio ya wengi zinaonesha mafanikio tu, hazioneshi nyakati ambazo wameshindwa, tena mara nyingi mno kabla ya kufikia mafanikio. Hivyo wewe unapojaribu kile walichofanya wao na ukashindwa, unaona labda wewe una mapungufu fulani, iweje wao walifanikiwa na wewe unashindwa?
Huna mapungufu yoyote rafiki, hata hao unaowaangalia sasa, walishindwa mara nyingi kabla hawajafanikiwa. Hivyo usitegemee wewe utaweza kufika walipofika bila ya kushindwa.
Ninachokushauri ni hiki rafiki yangu, amua ni nini unataka, kisha peleka kila rasilimali uliyonayo kwenye kupata kile unachotaka. Ukishindwa fanya tena, ukishindwa fanya tena, na tena na tena na tena. Kama upo hai, basi endelea na mapambano ya kupata kile unachotaka, wakati huo ukikazana kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa siku za nyuma na kutokurudia makosa yaliyopelekea wewe kushindwa.
Kama bado upo hai, na una nia ya kuendelea na mapambano, bado hujashindwa, usikiri kushindwa, ushindi ni wako kama hutokata tamaa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Hakika nitashindwa lakini sitorudi nyuma nitaendelea na safari yangu ya mafanikio.
LikeLike
Vizuri sana na kila la kheri.
LikeLike
Habari Makirita, nina shida nikiwa kwenye profile yangu nikifungua Makala yoyote kwenye read more iko faint hivyo nashindwa kusoma Makala hadi mwisho.
LikeLike
Salama,
Naomba uchukue screenshot halafu unitumie kwa wasap niweze kuona shida unapata wapi.
Karibu.
LikeLike