Kila kitu kinachotokea kwenye maisha yako, kuna manufaa ambayo yapo ndani ya kitu hicho. Hata kama ni kitu unachoona ni kibaya au kigumu.
Ugumu au changamoto unayopitia sasa, ina manufaa ndani yake, unaweza usione hilo wazi, lakini kwa kupitia ugumu au changamoto hiyo, unaweza kujiepusha na mambo mengine makubwa zaidi.
Makosa mbalimbali unayoyafanya kwenye maisha yako, yana manufaa ndani yake. Unaweza kunufaika zaidi na makosa unayofanya kuliko mafanikio ambayo unayapata.
Kabla hujalalamikia chochote, kabla hujaona kile unachokutana nacho ni kikwazo kwako, jiulize kwanza ni manufaa gani ambayo kitu hicho kimebeba. Angalia ni kwa namna gani kile kilichotokea kinakuzuia na makubwa zaidi ambayo yangeweza kutokea. Angalia ni kwa namna gani kinakupa funzo ili wakati mwingine usirudie tena kile ulichofanya.
Hupaswi kuwa mtu wa kulalamika au kulaumu juu ya kitu chochote, badala yake unapaswa kuwa mtu wa kuvuna manufaa kwenye kila kinachotokea kwenye maisha yako. Swali lako kuu linapaswa kuwa ni manufaa gani yako kwenye kitu hiki, kisha kuwa tayari kujifunza na kuyaona manufaa hayo.
Kila ugumu, kila kikwazo, kila makosa yanakuja na manufaa makubwa ndani yake. Hutaweza kuyajua na kunufaika nayo kama hutakuwa mtu wa kuyatafuta manufaa hayo. Kazi ni kwako sasa kuhakikisha kila unachopitia unayajua manufaa yake kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,