“Fortune falls heavily on those for whom she’s unexpected. The one always on the lookout easily endures.”
—SENECA, ON CONSOLATION TO HELVIA, 5.3
Ni siku nyingine mpya, siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Tumeipata nafasi hii nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA,
Mwongozo wetu ni AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA,
Msimamo wetu ni KAZI, UPENDO NA HUDUMA.
Kwa kusimamia maeneo hayo matatu, siku ya leo itakuwa bora sana kwetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UTAUMIA KAMA HUTARAJII…
Asili huwa inafanya mambo yake kwa namna inavyochagua yenyewe,
Sisi huwa ni wapokeaji tu wa matokeo ya kile ambacho asili imefanya.
Sasa, watu wengi sana wamekuwa wanaumia na matokeo ambayo asili imewaletea,
Na wanaoumia sana ni wale ambao hawakutarajia kitu fulani kitokee.
Mfano kama una mtu wako wa karibu ambaye ameumwa na kulala kitandani hoi kwa mwezi mzima, mara kadhaa akakata kauli na kuzidiwa, ukisikia amefariki utaumia.
Lakini kama una mtu wako wa karibu ambaye asubuhi umeongea naye na mkaagana vizuri huku mkiwa na mipango ya kufanya kitu fulani baadaye, halafu saa moja baadaye ukapewa taarifa kwamba amepata ajali na kufariki hapo hapo, utaumia zaidi.
Sasa hawa ni watu wa karibu na wote wamefariki, lakini mmoja umeumia kiasi na mwingine umeumia zaidi, hii inatokana na nini?
Hii inatokana na matarajio,
Kwa yule aliyeugua sana, ukishaanza kuwa na matarajio kwamba atafariki, maana amekuwa hoi kwa muda mrefu.
Lakini yule aliyefariki kwa ajali ghaflam hukuwa na matarajio kwamba anaweza kufa siku hiyo, na hivyo unaumia zaidi.
Wastoa wanatuambia kuondokana na hali hii, tuwe tunatengeneza matarajio ya chochote kinachoweza kutokea, ili kinapotokea tusishangazwe wala kuumizwa sana.
Lakini pia kwa kuwa na matarajio hayo, unakitumia vizuri kitu wakati bado unacho.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuwa na matarajio kwamba chochote kinaweza kutokea kwako na kwa wengine pia hivyo kutokuumia sana pale kinapotokea, lakini pia kutumia vitu vizuri wakati bado unavyo.
#TarajiaUsiyotarajia #AsiliHaikufuatiWewe #KushangazwaNiKukosaMaandalizi
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/makirita3.1