Siku zote mtu ambaye hajaoa au kuolewa anaweza kuona mchezo wa ndoa vizuri na kuelewa kuliko mwanandoa mwenyewe. Watu ambao hawajaoa au kuolewa ni kama vile makocha wa timu, mchezaji anapokuwa uwanjani hawezi kuona makosa yake lakini yule anayemfundisha na kumwangalia anajua wapi  uimara wake uko na udhaifu.

Unaweza kuona mchezo wa ndoa ni mrahisi au mgumu kadiri ya mitazamo yako na yule ambaye yuko nje kama kocha akiingia ndani ya mchezo wa ndoa hawezi tena kuyaona yale aliyokuwa anayaona kama alivyokuwa kocha.

Ndoa nzuri siyo pale wanandoa waliokamikika kuwa pamoja bali ni pale wanandoa wasiokamilika kujifunza na kufurahia tofauti zao.

Hatuwezi kusema kuna mtu ambaye anaweza kuwa amekamilika, sisi wote hatujakamilika kwani kila mtu ana madhaifu yake hivyo basi, tukiweza kuchukuliana haya madhaifu yetu ndiyo yanapelekea ndoa nzuri.

Aliyekuwa baba wa falsafa Socrates aliwahi kusema neno juu ya ndoa na hivi ndivyo alivyosema ‘’ kwa namna yoyote ile oa au olewa, kama ukimpata mke mwema utakua na furaha lakini kama ukimpata mke mbaya , ambaye si mwema au mzuri kitabia utakua mwanafalsafa. Hayo ndiyo maneno ya Socrates.

Kwa uhalisia ninakubaliana na Socrates kwani ukiwa na mke au mume mwema hapa tunaangalia zile zifa za kuwa mke au mume bora utakua na maisha ya furaha katika ndoa yako. Tunashuhudia misemo mbalimbali ikisema  kosea kujenga lakini siyo kukosea kuoa au kuolewa.

Image result for by all means marry if you get a good wife

Ukikosea kujenga unaweza ukabomoa na kujenga upya vipi kama  ukikosea mke au mume?

Unaalikwa kumtafuta mtu ambaye ana tabia nzuri, ambaye unajua mnaweza kuvumiliana na kuendana kadiri ya tabia zenu hapo mtakua wanandoa wenye furaha.

Ukimuoa au kuolewa na mtu ambaye siyo, yaani tabia ni mbaya utashindwa mapema  kwani ni rahisi kumfundisha mtu kazi lakini siyo tabia.

Vipi sasa kwa upande wa mwanamke au mume ambaye siyo mwenye tabia nzuri, Socrates yeye amesemaje?

Mtazamo wake Socrates ni kwamba ukimpata mtu ambaye siyo sahihi katika ndoa basi utaishia kuwa mwanafalsafa.  Kwanini amesema utaishia kuwa mwanafalsafa?

Ni kwa sababu kupitia zile changamoto utakazozipitia zitakufundisha na kufikiria kama vile mwanafalsafa anavyoumiza kichwa kufikiri. Kwa lugha ya mtaani wanasema ukiwa na mke au mume ambaye siyo sahihi huna rangi ambayo hutaacha kuiona.

Kama unataka kuwa mwanafalsafa bila kupenda basi oa au olewa na mtu ambaye siyo sahihi kwako. Matatizo ambayo yanakuwa yanawasumbua watu kwenye maeneo mbalimbali yanapelekea watu kuwa wanafalsafa wa matatizo hayo. Yale matatizo yanawatengeneza watu na kisha kuwafundisha jinsi wanavyopaswa kuwa.

Hatua ya kuchukua leo; tafuta mke au mume mwenye tabia nzuri hapo utakua na ndoa yenye furaha lakini kama hutaki chukua yoyote na utakua mwanafalsafa. Iko misingi bora ya jinsi ya kumpata mke makini na hii utaweza kuipata kwenye vitabu au watu waliofanikiwa waliwezaje kupata watu makini. Kwa kukusaidia rafiki yangu, nakusihi usome kitabu cha Ijue Njaa Ya Wanandoa.

SOMA; Ushauri Kwa Kijana Yeyote Anayetaka Kuingia Katika Mahusiano Ya Ndoa

Kwahiyo, ndoa siyo mbaya wala nzuri uzuri au ubaya wa ndoa uko kwenye tafsiri ya mtu mwenyewe. Ile mitazamo ambayo mtu anaitoa ndiyo inampelekea kupata kile anachoamini. Kwahiyo, ndoa  ni nzuri au mbaya kadiri ya mtazamo wako ulionao juu ya ndoa.

Kama ingekuwa mbaya kwanini watu wanaendelea kuoana kila siku? Na kama ingekuwa nzuri kwanini watu wanaendelea kuachana na kutalakiana?  Tumia akili na usifuate mikumbo ya watu linapokuja suala la ndoa.

Makala hii imeandikwa na

Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa  http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl. Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com

Asante sana